Wanawake Ilala wataja sababu kumuunga mkono Rais Samia

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:43 PM Jun 15 2025
Rais Samia Suluhu
PICHA: MTANDAO
Rais Samia Suluhu

SABABU 12 zilizotangazwa na Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, zimetosha kutoa maazimio ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba mwaka huu.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Rehema Sanga ametangaza uamuzi huo wakati wa kongamano la wanawake wajasiriamali wa Jiji hilo lililofanyika jana jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa sababu alizozitaja ni Rais Samia amekuwa mbeba maoni na mtetezi mkubwa wa wanawake na kulifanya suala hilo kuwa nguzo muhimu ya kujikwamua kiuchumi.

“Ameonesha kwa vitendo azma yake ya kumkomboa mwanamke kiuchumi kwa kurejesha mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu na kuboresha mfumo wa upatikanaji jumuishi kwa kushirikiana na benki,” amesema Rehema.

Vilevile amesimamia maboresho ya sheria ya Ununuzi wa Umma sura ya 410 Ibara ya 35(1) (6) inayotoa kupaumbele kwa makundi maalum yakiwamo wanawake kupata asilimia 30 ya manunuzi ya taasisi zote za umma.

Aliitaja pia sababu ya mabadiliko ya Sera ya Elimu na kuhakikisha wanafunzi wanasoma bila kulipa ada kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita, kusimamia upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kujenga miundombinu ya afya kama hospitali, vituo vya afya na zahanati kila mahali na kununua vifaa tiba vya kisasa.

“Amekuwa kinara wa Afrika na dunia kuhusu uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia, imesaidia kuondoa athari zitokanazo na moshi kwa wanawake na jamii vilevile kupunguza gharama za  mkaa na kuni, ameleta programu ya M- Mama ambayo imepunguza vifo vya mama na mtoto kupitia jitahada hizo amepata Tuzo ya Gates Goalkeeper kutoka Taasisi ya Bill and Melinda Gates,” amebainisha Rehema.

Ameongeza kuwa  Mkuu huyo wa Nchi amekuwa jemedari wa kusimamia na kulinda tunu za taifa  ambazo ni   utu, umoja, uzalendo, uwajibikaji, maadili kwa lugha ya kiswahili ambazo ndio msingi wa maadili na uimara wa utamaduni wetu.

Aidha amesema  kupitia falsafa yake ya 4R imeleta mafanikio makubwa kwenye  uongozi kwa kujenga Tanzania bora yenye maridhiano  na maelewano na hivyo kuleta mabadiliko chanya ndani ya taifa katika nyanja za kijamii, kisiasa, na kiutamaduni.

MAAZIMIO

Kupitia sababu  hizo jukwaa hilo, liliazimia kumuunga mkono na kusimama imara kuongoza taifa na kusimama imara nyuma yake pia kuunga mkono juhudi zake katika kujenga tanzania kuelekea taifa lenye  amani, utulivu, ustawi,  na Maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Amesema watatangaza mafanikio yake kwa kupita nyumba kwa nyumba kuwashawishi watanzania wote wamuunge mkono na kumpigia kura katika uchaguzi ujao pamoja na Kuhakikisha anapata kura za kishindo ili aendelea kuliongoza taifa kwa kipindi cha  miaka mingine mitano.