Serikali yataka shule binafsi kuzingatia ICT kwenda na wakati

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 03:52 PM Jun 15 2025
Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi wa Wizara ya Elimu Alhaji Abdul Maulid.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi wa Wizara ya Elimu Alhaji Abdul Maulid.

Serikali imepongeza mchango wa shule binafsi katika elimu na imezitaka shule hizo kwenda sanjari na mabadiliko ya teknolojia duniani ili kutoa wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiri wenzao.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolph Mkenda, kwenye hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi wa Wizara hiyo, Alhaji Abdul Maulid.

Alikuwa akizungumza jijini Dar es Salaam kwenye sherehe ya maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule za Green  Acres.

Alisema mbali na kodi kwa serikali na kuongeza ajira shule hizo zimekuwa zikiongeza fursa kwa watanzania kupata elimu bora kwani yenyewe isingekuwa na uwezo wa kusomesha watanzania wote.

Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuwa siku zote amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha elimu inaboreshwa na kutoa wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.

“Ni muhimu kukumbuka kuwa ni kupitia maono ya Rais Samia tumefanikiwa kufanya maboresho ya sera ya elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 sera ina mambo mengi mazuri sana,” alisema

Aliipongeza shule hiyo kwa kuwalea wanafunzi kwenye mazingira ya uadilifu na uzalendo nidhamu na maadili kwa wanafunzi wake.

“Nyote ni mashahidi wa namna gani maadili imekuwa changamoto kubwa lakini nafurahi sana kusikia kwamba mmewekeza sana kwenye masuala ya nidhamu na maadili,” alisema

 “Mafanikio yote haya hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa walimu, menejimenti, wazazi na wanafunzi na ndiyo maana wanafunzi wengi waliohitimu Green Acres wana maadili na wanafanya vizuri sehemu zao za  kazi,” alisema

Alisema serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika elimu na itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wadau hao ili kuleta ustawi zaidi katika kutoa huduma kwa umma.

“Tunajua kuna changamoto lakini serikali haiwezi kuwaacha, kila litakapotokea jambo tutawaalika tujadiliane namna ya kutatua changamoto,” alisema

Aidha, alisema shule binafsi zikiwemo za dini zimekuwa na mchango mkubwa sana kwenye upatikanaji wa elimu nchini na zimekuwa chachu ya ushindani kwenye maendeleo ya elimu nchini.

“Sekta binafsi kwenye elimu mnatoa mchango mkubwa sana kwenye kodi, ajira na shule binafsi zinaongeza fursa za elimu kwa watanzania na nimefurahi kusikia mbali na wanaolipa mnachukua baadhi ambao hawana uwezo mnawasomesha,” alisema

“kuna yatima, kuna ambao ni maskini na wengine wazazi wao  ni wagonjwa wa muda mrefu lakini Green Acres mmewachukua na ndiyo maana mnazidi kuwa juu kitaaluma kwa kutoa elimu bora,” alisema.

Aliwapongeza piaa kwa kuanzisha utaratibu wa kusomesha watoto 15 wasiojiweza kila mwaka kama mkakati wa kurejesha faida kwa jamii.

Mkurugenzi wa shule hizo, Jackyline Rushaigo alisema kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu kama wale wenye ulemavu wa ngozi ambao wamekuwa wakiwapokea na kuwasaidia kielimu kwa kuwasomesha bure.

“Tumeona umuhimu wa kusaidia jamii kusomesha watoto hawa na kila mwaka kwenye shule zetu zilizoko mkoa wa Dar es Salaam na Kagera tunachukua wachache tunawasomesha bure,” alisema

Aidha, Jackyline aliipongeza serikali kwa kuanzisha mitaala mipya ya elimu ambayo alisema inawasaidia wanafunzi kusoma zaidi kwa vitendo bafala ya nadharia kama zamani.

“Mitaala hii mipya imeleta hamasa kubwa sana kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi badala ya kukaa darasani pekee, hii inainua vipaji sana kwani wanasoma kwa vitendo na inamwezesha mwanafunzi kujua anachopenda na kubobea mapema,” alisema