Serikali kuendelea kuboresha ustawi wa maisha ya wazee

By Marco Maduhu , Nipashe Jumapili
Published at 06:01 PM Jun 15 2025
Wazee
PICHA: MARCO MADUHU
Wazee

NAIBU Waziri Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,wanawake na makundi maalumu Mwanaidi Khamis,amesema serikali itaendelea kuboresha ustawi wa maisha ya wazee, pamoja na kuwapatia huduma zote stahiki.

Amebainisha hayo leo Juni 15,2025 wakati akitoa hotuba kwenye uhitimishaji wa siku ya kitaifa ya kuelimisha na kupinga ukatili dhidi ya wazee,maadhimisho ambayo yamefanyika mkoani Shinyanga.

Amesema serikali inatambua na kuthamini mchango wa wazee hapa nchini, na imekuwa mstari wa mbele kuratibu na  na kusimamia utekelezaji wa afua zinazotoa kipaumbele katika kuimarisha huduma za wazee na kuboresha ustawi wa maisha yao.

 “Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi yam waka 2022 Takwimu zinaonyesha kuwa kuna jumla ya Wazee Milioni 3.4 na kutokana na Takwimu hizi, Serikali imeendelea kuwafanyia Jitihada mbalimbali ili kuhakikisha kundi hili linapata huduma stahiki na kuboresha ustawi wa maendeleo maisha yao,”amesema Mwanaidi.

 Aidha,ametaja miongoni mwa maeneo ambayo yamepewa kipaumbele na Serikali katika kuwahudumia wazee, ni utoaji wa huduma za Afya kwa kuwapatia matibabu bila malipo, na kwamba  kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 mpaka Aprili 2025,Wazee Milioni 2.1 wamepatiwa Vitambulisho vya Bima ya Afya CHF iliyoboreshwa kwa ajili ya matibabu bure.

 Amesema pia kupitia Kampeni ya Mpishe Mzee kwanza apate huduma kwenye huduma za Afya, kwamba hadi sasa kuna jumla ya madirisha 4,574 ya kutolea huduma za Afya za Msingi kwa Wazee katika Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya.

 Amesema serikali itaendelea kutoa huduma za matunzo kwa wazee waasiojiweza kupitia makazi ya wazee 13,ambayo yanamilikiwa na kuendeshwa na serikali yenye wahudumu 233.

 Katika hatua nyingine amesema serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji dhidi ya Wazee,huku akitaja takwimu za mauaji ya wazee kwamba mwaka 2022 yalitokea 130, ambapo mwaka 2023 yalikuwa 152, na mwaka 2024 yalipungua yakiwa 138.

 “Natoa wito kwa jamii kuacha kabisa kufanya matendo yanayoashiria ukatili dhidi ya wazee,bali wanapaswa kulindwa,kuthaminiwa na kuhudumiwa,amesema Mwanaidi. Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro,akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.amekemea tabia ya baadhi ya vijana kuwatelekeza wazee wao na kuwaacha wakiishi maisha ya tabu, huku wengine wakiwa wamekaa nyumbani bila kazi na kuelelewa na wazee.

 Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa, David Sendo akisima risala ya wazee, wameiomba serikali kuendelea kuwatimizia mahitaji yao ikiwamo huduma bora za afya,pamoja na kuwatungia sheria ya wazee na siyo kuendelea kuishi kwa sera yam waka 2003.

 Pia,wameomba kudhibitiwa kwa Waganga ambao wamekuwa wakipiga Ramli Chonganishi na hata kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia,ambapo kipindi hiki cha uchaguzi Mkuu matukio hayo ndiyo hushamiri kwa wingi. Kauli Mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Wazee ya kuelimisha na kupinga ukatili dhidi ya wazee duniani inasema “Wazee ni Hazina kwa Taifa,Tuwalinde na Tuwatunze”