Katika jitihada za kuhakikisha kuwa Serikali inapata thamani halisi ya fedha katika miradi yake, Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewasihi wazabuni kushiriki mafunzo yanayoratibiwa na Mamlaka hiyo ili kuwajengea uwezo wa kutumia Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando pembezoni mwa Kongamano la Tisa la Ununuzi wa Umma la Mwaka 2025 linaloendelea Jijini Arusha. “Moduli hii imejengwa ili kusaidia umma na hususan kuendana na miongozo ya Serikali ya kuzitaka taasisi za umma kutumia tehama katika kufikisha huduma zake kwa wananchi kwa wakati uliokusudiwa,” amesema Sando
Baada ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuzindua rasmi matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia Malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST mwezi Februari 2025, Mamlaka ya Rufani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendelea za zoezi la kutoa mafunzo mahususi ya matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kieletroniki katika Kanda mbalimbali nchini.
“Katika kuhakikisha wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma wanapata mafunzo ya matumizi ya moduli PPAA imeendelea na zoezi la kutoa mafunzo mahususi ya Moduli katika kanda mbalimbali ambapo hadi sasa Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zimepatiwa mafunzo hayo,” amesema
Sando
Aidha, Sando ameongeza kuwa hadi sasa PPAA imefanikiwa kutoa mafunzo kuhusu matumizi ya moduli hiyo kwa wazabuni 800 na wakuu wa Idara/Vitengo vya ununuzi na sheria wapatao 1,588 kutoka katika taasisi nunuzi 500.
Sando ameongeza kuwa matumizi ya moduli yana faida nyingi zikiwemo mzabuni kutolazimika kufika katika ofisi za taasisi nunuzi au za PPAA ili kuwasilisha lalamiko au rufaa yake. Kadhalika, inasaidia kupunguza gharama na muda kwa wazabuni kwani hawatalazimika kusafiri ili kuweza kuwasilisha malalamiko au rufaa zao PPAA.
“Moduli inaongeza uwazi katika mchakato wa ushughulikiwaji wa malalamiko na rufaa kwa kuwa mzabuni aliyewasilisha lalamiko au rufaa lakini pia ataweza kuona hatua mbalimbali za ushughulikiaji wa lalamiko au rufaa yake, na kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu za taarifa za malalamiko na rufaa,” amesema Sando
Kadhalika, Sando amewasihi wazabuni kutoka mkoa wa Dodoma na mikoa jirani kushiriki mafunzo mahususi kuhusu Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki katika mfumo wa NeST yatakayofanyika katika ukumbi wa Lavenda Hall tarehe 18 Juni 2025 Jijini Dodoma.
Awali, akitembelea mabanda ya maonesho katika viwanja vya Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) kabla ya kufungua rasmi Kongamano la tisa la Ununuzi wa Umma la Mwaka 2025, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima aliipongeza PPAA kwa kuanzisha Moduli ya kupokea na kushughulikia Malalamiko na Rufaa kieletroniki.
Pamoja na mambo mengine, Dk. Gwajima aliahidi kuwa balozi wa hiari wa kuinadi Moduli ya kupokea na kushughulikia Malalamiko na Rufaa kieletroniki kwa wadau wa ununuzi hususan Wanawake na Makundi Maalum.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED