Katika jamii ya Kitanzania, baba huchukuliwa kama kiongozi, mlinzi, na mhimili wa familia. Huyu ni mtu anayebeba ndoto za familia yake mabegani, mara nyingi bila kulalamika. Ingawa upendo wa baba mara nyingi hujieleza kwa vitendo kuliko maneno, mchango wake ni wa kipekee na hauwezi kupuuzwa.
Tunapoadhimisha Siku ya Baba, tunatazama nafasi hii kwa jicho la shukrani, lakini pia la kutafakari. Tunapopongeza na kusherehekea juhudi za baba zetu, hatuwezi kufumbia macho changamoto zinazowakumba katika dunia ya sasa dunia ambayo imebadilika kwa kasi na kuweka mzigo mpya juu ya mabega yao.
KIMYA CHENYE MAANA
Miaka ya nyuma, baba wa Kitanzania alikuwa ni mtu wa heshima kubwa, mwenye usemi wa mwisho katika familia. Alijulikana kwa ukimya wake, kwa ukali wake wa malezi, na mara nyingi kwa utulivu wake wa kihisia. Lakini ndani ya ukimya huo kulikuwapo na upendo, wajibu, na dhamira.
Baba wa enzi hizo alikuwa mtu wa kujitoa kwa kazi; akiamka mapema, akifanya kazi shambani au kazini mchana kutwa, na kurudi nyumbani akiwa amechoka. lakini bado na moyo wa kuwajali watoto wake.
Malezi yalikuwa ya nidhamu kali, lakini kwa misingi ya kukuza heshima, utu na uwajibikaji. Alifundisha kwa mfano, si kwa hotuba. Hakusema 'nakupenda', bali alihakikisha una viatu shuleni. Baba aliishiwa soksi lakini hakukosa ada alitoa alichonacho kwa upendo usio na masharti. Alikosea wakati mwingine, lakini nia yake daima ilikuwa njema kuona familia ikifaulu zaidi yake.
BABA WA LEO
Kama kuna jambo moja ambalo Siku ya Baba linapaswa kutufundisha, ni kwamba kuwa baba leo si kazi ndogo. Dunia imebadilika, mahitaji ya familia yamebadilika, watoto wamebadilika na kwa namna fulani baba naye analazimika kubadilika.
Lakini mabadiliko hayo hayaji kwa urahisi. Kwa nyuma ya tabasamu lake na ukimya wake wa kawaida, baba wa leo anapambana na mzigo mkubwa zaidi kuliko tunavyofikiria.
Baba si tena mtu wa kuogopwa, anayetoa amri kutoka kona ya sebuleni. Katika mazingira ya sasa, baba si tu mtafutaji wa riziki. Anatarajiwa pia kuwa mlezi wa kihisia, mshauri wa familia, mwanaume mwenye nguvu lakini pia huruma, anayesoma alama za nyakati na kukua pamoja na watoto wake. Lakini safari hiyo imejaa changamoto nyingi ambazo kwa muda mrefu zinafichwa au kupuuzwa.
UKWELI USIOANDIKWA WALA KUSIMULIWA
Wakati tunasherehekea ubaba wa kisasa, ni muhimu pia kutambua kwamba viatu anavyovaa baba wa leo ni vizito kuliko vinavyoonekana. Zifuatazo ni baadhi ya changamoto zinazowakabili mababa wengi katika ulimwengu wa leo changamoto ambazo haziandikwi kwenye kadi za shukrani, lakini zimejaa kwenye mioyo yao:
· Msongo wa Kiakili na Kisaikolojia
Katika harakati za kutimiza wajibu wa kifamilia na kijamii, baba wa leo anakumbana na msongo wa mawazo mkubwa. Anatakiwa kuwa mtafutaji wa kipato, mlezi, mume bora, na bado asionyeshe dalili za kuchoka. Mara nyingi hana nafasi ya kutoa hisia zake au kuomboleza machungu yake.
Kwa baadhi ya wanaume, kuficha hisia huonekana kama ishara ya ‘uanaume’. Lakini ndani, wengi wanavunjika kimya kimya. Hili limechangia kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili kwa wanaume, ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo na huzuni ya muda mrefu.
· Ukimya wa Unyanyasaji wa Kinyumbani kwa Wanaume
Ni jambo lisiloelezwa sana, lakini linazidi kujitokeza: baadhi ya wanaume wanapata manyanyaso kutoka kwa wake zao kisaikolojia, kihisia, na wakati mwingine hata kimwili. Hawawezi kusema kwa kuhofia aibu au dharau kutoka kwa jamii.
Mwanaume anayepigwa au kubezwa mara kwa mara anaweza kuishi kwa mateso makubwa, lakini bado anatarajiwa kuwa "imara." Siku ya Baba iwe pia siku ya kusema: unyanyasaji hauna jinsia, na mwanaume naye anahitaji usaidizi anapojeruhiwa.
· Teknolojia na ulimwengu wa kidijitali
Mitandao ya kijamii, na utandawazi vimeleta mabadiliko makubwa katika mahusiano ya kifamilia. Watoto sasa wanakulia kwenye dunia ya vifaa vya kidijitali ambapo sauti ya TikTok inasikika kuliko sauti ya baba.
Baba wa leo anajikuta akishindana na mitandao kama YouTube, Instagram, Facebook au hata marafiki wa mtandaoni kuweza kuwasiliana na watoto wake. Wakati mwingine, anajihisi kutengwa au kutokuwa na ushawishi tena kwenye maisha ya watoto wake.
Zaidi ya hapo, teknolojia imeingilia hata muda wa familia kila mtu akiwa kwenye kifaa chake. Mazungumzo mezani yamepungua, na nafasi ya baba kama mlezi wa maadili imeingia mashakani. Anatakiwa kujifunza teknolojia ili asiwe mbali na dunia ya watoto wake, bali awe sehemu ya mwongozo wao mtandaoni.
· Mabadiliko ya kijinsia na nafasi ya mwanaume
Dunia inapoendelea kupaza sauti za haki za wanawake ambayo ni hatua chanya na ya msingi kuna baadhi ya wanaume wanaohisi kama nafasi yao imeanza kufifia. Wengine huchanganyikiwa kuhusu nafasi yao katika familia au jamii.
Lakini uhalisia ni kwamba, dunia ya leo inahitaji usawa, si ushindani wa kijinsia. Inahitaji wababa wanaoweza kuwa mfano bora wa usawa, huruma, na uwajibikaji.
Mwanaume wa leo anatakiwa kujifunza kushirikiana badala ya kutawala. Ubaba mpya unahitaji moyo wa kujifunza upya, kukubali mabadiliko ya kijamii, na kushiriki majukumu bila hofu ya kudharaulika. Ni kupitia usawa huu ndipo watoto hujifunza kuheshimu kila jinsia kwa vitendo, si maneno tu.
· Umasikini na ugumu wa maisha
Katika baadhi ya familia, baba anatafuta kazi kwa miezi au miaka bila mafanikio. Anakosa uwezo wa kutoa mahitaji ya msingi kwa familia yake. Hii humfanya ajihisi kushindwa, na wakati mwingine kukataliwa na familia au jamii.
Ni muhimu kutambua kuwa thamani ya baba haiwezi kupimwa kwa pesa pekee. Wapo mababa maskini lakini waliojaa hekima, mapenzi, na moyo wa kujitoa.
Wanapojitahidi kwa kila hali bila kuona matunda ya haraka, hubeba mzigo wa aibu kimya kimya. Baadhi yao hujikuta wakikimbilia pombe au kujitenga kijamii kutokana na msongo wa mawazo. Baba wa aina hii anahitaji uelewa, si hukumu anahitaji kupewa matumaini, si kuachwa nyuma.
Kukamilishana siyo kushindana
Tunaishi katika zama ambazo wanawake nao wanafanya kazi na kuchangia kipato cha familia na hilo ni jambo la kujivunia. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa nafasi ya mwanaume katika familia bado ni ya msingi.
Mume kutokuwa na kazi au kuwa na kipato kidogo hakupaswi kuondoa heshima yake kama kichwa cha familia. Wanaume wasione aibu, kwani jukumu lao si pesa pekee, bali ni kuongoza kwa hekima na kutunza familia. Vivyo hivyo, wanawake wanapaswa kutambua kuwa mafanikio ya kifedha hayaondoi nafasi ya mwanaume.
Kama jamii, tukianza kupima thamani ya baba kwa pesa, tunawaharibu watoto wetu. Watoto hujifunza kwa kuona na wakiona baba akiheshimiwa hata bila ajira, wanajua thamani ya utu. Wakiona mama akimpa nafasi baba, wanajifunza kushirikiana, si kushindana.
Ubaba si mashindano ya kipato. Ni kujitoa, kuongoza kwa upendo, na kujenga familia yenye maelewano msingi wa jamii imara ya kesho.
KUMTAMBUA BABA NI ZAIDI YA ZAWADI
Siku ya Baba isiwe tu ya kumnunulia kofia au soksi. Iwe siku ya kusikiliza sauti yake, kuelewa kilio chake kisicho na machozi, na kutambua mchango wake kwa jicho jipya.
Tuwaambie: Baba, hatujakusahau. Tunajua umevumilia. Tunajua hujasema kila kitu. Tunakuona, tunakuthamini.
Tuchukue muda kumwuliza hali yake, si tu kama mzazi bali kama mwanadamu anayeweza pia kuchoka. Tumpongeze hadharani, tuwaambie watoto wake jinsi alivyo shujaa. Tukumbuke kuwa hata mgongo wa simba huwa na majeraha, lakini bado huinua kichwa kwa fahari na kupigania walio kwenye himaya yake.
BABA NI SHULE YA MAISHA
Baba ni darasa lisilofungwa. Kupitia yeye tunajifunza ujasiri, uvumilivu, maamuzi magumu, na kujitolea. Anapotenda kwa uadilifu, watoto wake huiga. Anapokosea na kukubali, watoto hujifunza unyenyekevu. Ubaba si ukamilifu ni kujitahidi kila siku kuwa bora kwa ajili ya wengine.
Ni mwalimu anayefundisha kwa maisha, si maneno pekee. Mafanikio ya watoto wake ni ripoti yake ya kila mwaka. Anaweza kuwa hajawahi kuandika insha kuhusu upendo, lakini matendo yake huandika riwaya nzima ya kujali. Kila hatua anayochukua huwa somo lisilosahaulika kwa watoto wake.
MSINGI USIOONEKANA
Katika jamii yetu ya Tanzania, baba ni msingi wa familia, hata kama misingi hiyo haionekani kwa macho. Ni mtu ambaye mara nyingi haitaji sifa, lakini maisha ya watoto wake yanakuwa ushahidi wa upendo wake.
Katika dunia ya leo yenye changamoto, wababa wanahitaji kusikilizwa, kuthaminiwa, na kusaidiwa. Kwa wababa wote wale waliopo, waliotangulia, waliopigana kimya kimya, au waliopoteza mwelekeo na wanatafuta kurudi tunawaambia: Asante kwa kuwa nguzo, taa, na kioo cha familia.
Siku Njema ya Baba. Ustahili upendo wetu leo na kila siku. Ulimwengu unaweza kusahau jina lako, lakini watoto wako hawatasahau kujitolea kwako. Umejenga urithi usio na majengo umewaacha watu waliokomaa, wenye upendo, maadili na moyo wa kujituma. Katika kila hatua yao, kuna kivuli chako kikiwapa mwelekeo.
Kwa maoni wasiliana na judithjamestz@gmail.com
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED