Polisi waanika kilichojificha matukio ya wizi wa watoto

By Waandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 08:52 AM Aug 25 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa.

MAKAMANDA wa Polisi Mikoa ya Mwanza na Shinyanga wamesema uchunguzi wa muda mrefu umebaini matatizo ya uzazi katika familia ndicho chanzo cha matukio ya wizi wa watoto.

Wamesema hali hiyo ni tofauti na imani potofu zilizojengeka miongoni wa jamii zikihusisha matukio ya watoto kupotea na masuala ya imani za kishirikina pamoja na Uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, aliyasema hayo wakati akitoa taarifa ya kumkamata George Mlalo (21), mkazi wa Kisiwa cha Kamasi, wilayani Ukerewe, mkoani humo, kwa tuhuma za wizi wa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na kuishi naye. 

Alisema sehemu kubwa ya watuhumiwa wanapokamatwa wamekuwa wakitaja kukosa watoto katika ndoa zao na hivyo kutamani kuiba watoto. 

"Sababu hii imekuwa ikijitokeza katika matukio tunayokamata wanaume kwa wanawake. Hali hiyo inachangiwa na lawama na migogoro ya kukosa watoto ndani ya ndoa," alisema Kamanda Mutafungwa. 

Alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mvuvi, alikamatwa Agosti 16 mwaka huu, saa moja jioni katika Kisiwa cha Ghana, wilayani Ukerewe kwa tuhuma za kumuiba mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja (jina tunalo), mkazi wa Kisesa, wilayani Magu, kwa madai kuwa alimpenda na kuamua kuishi naye. 

"Mtoto tumemfanyia uchunguzi na tumebaini kuwa yupo salama, hivyo kumrejesha kwa mama yake Irine Festo (22), na mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo," alisema Kamanda Mutafungwa. 

Katika tukio lingine, Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kukamatwa kwa Hadija Juma (24), mkazi wa Kijiji cha Sengerema, wilayani Uyui, mkoani Tabora, kwa tuhuma za wizi wa mtoto wa kike. 

Kamanda Janeth alisema wizi huo uliotokea Agosti 20 mwaka huu, saa 12 jioni, katika Kituo cha Afya Ushetu, wilayani Kahama, mkoani humo. 

"Mtuhumiwa tumemhoji na amekiri kutenda kosa na sababu ni zilezile kwamba, amekuwa anaolewa lakini hajafanikiwa kuzaa na hadi sasa amefikisha ndoa ya pili na kuachika. Taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea," alisema Magomi. 

Alisema mtoto huyo alizaliwa Agosti 17 mwaka huu na taarifa za kuibwa zilitolewa polisi Agosti 21 katika Kituo cha Polisi Nyamilangano, Ushetu, ndipo ufuatiliaji ulipoanza na mtuhumiwa kukamatwa Agosti 22 mwaka huu, saa tatu usiku. 

*Imeandaliwa na Marco Maduhu (SHINYANGA) na Vitus Audax (MWANZA)