Chalamanda kuchukua mikoba ya Yacoub, JKT

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:57 PM Jul 20 2025
news
Picha Mtandao
Kipa wa Kagera Sugar, Ramadhani Chalamanda, kushoto.

KLABU ya JKT Tanzania imetajwa kukamilisha usajili wa kipa wa Kagera Sugar, Ramadhani Chalamanda ili kuziba nafasi ya kipa namba moja wa timu hiyo na timu ya taifa, Taifa Stars, Yacoub Suleiman, anayedaiwa kusajiliwa na Simba.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kipa huyo amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya kumaliza mkataba na timu yake hiyo ya zamani huku ikiwa imeshuka daraja.

"Kigezo tulichotumia ni uwezo wake binafsi, pamoja na kwamba timu yake imeshuka daraja, lakini Chalamanda ni mmoja kati ya makipa waliofanya vizuri msimu uliomalizika, bila kujali hatua ya timu yake kushuka daraja.

“Alikuwa mmoja wa makipa mwenye 'saves' nyingi, pamoja na kuokoa michomo ya penalti, tutakuwa naye kwenye timu yetu kwa msimu ujao na tunaamini kwenye kipaji chake," alisema mtoa taarifa.

Hivi karibuni, kipa huyo alikiri kuwa amemaliza mkataba na Kagera Sugar, huku akisema anaweza kuichezea timu yoyote ile ambaye atakubaliana nayo maslahi kwani kazi yake ni kucheza soka.

JKT Tanzania ni moja kati ya timu zitakazolazimika kufanya usajili mkubwa kutokana na wachezaji wao wengi kuhusishwa kusajiliwa na timu nyingine baada ya baadhi yao kuonyesha viwango vikubwa msimu uliomalizika.

Chalamanda anakwenda kuchukua nafasi ya Yacoub, ambaye inadaiwa kuwa tayari ameshakubaliana na Simba, huku pia ikitajwa, Wilson Nangu na Karim Mfaume nao pia kutimkia Msimbazi.

Maafande hao walimaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakiwa na pointi 36, wakiweka rekodi ya kuwa timu iliyotoa sare nyingi msimu uliomalizika, ikiweka rekodi hiyo kwa misimu miwili mfululizo.

Msimu uliomalizika, ilitoka sare mara 12, baada ya kucheza mechi 30, ikishinda nane na kupoteza mechi 10, ambapo msimu wa 2023/24 ilitoka sare mara 14.