TIMU ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, imeanza kampeni yake ya michuano ya CHAN 2024 kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani, Nairobi.
Bao hilo la ushindi lilifungwa na kiungo mshambuliaji Austin Odhiambo dakika ya 45 ya mchezo.
Katika mchezo huo wa kundi A, ambao ulipigwa Jumapili, Agosti 3, Harambee Stars walionyesha ujasiri na mbinu kali tangu mwanzo. Pambano hilo lilikuwa la kasi, huku timu zote mbili zikishambuliana kwa zamu.
DRC walionekana kuwa na kasi na nguvu, lakini walikosa umakini katika kumalizia mashambulizi yao. Hata hivyo, Kenya walijilinda vizuri na walifanikiwa kutumia nafasi waliyoipata.
Ushindi huu unaipa Kenya matumaini makubwa katika hatua ya makundi, ambapo inajiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele. Odhiambo, ambaye alifunga bao hilo muhimu, alipokea sifa kutoka kwa mashabiki na wataalam wa soka kwa utulivu na weledi wake.
Jana wenyeji wengine Tanzania, iliichapa Burkina Faso 2-0 jijini Dar es Salaam. Kesho wenyeji wengine Uganda watajiuliza kwa Algeria kwenye Uwanja wa Mandela, Kampala.
Chanzo: BBC
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED