Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema michuano ya CHAN inayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti, mwaka huu ni zaidi ya michezo kwasababu yanafungua fursa za kibiashara na uchumi.
Museveni ameyasema hayo jana katika eneo la Kilolo nchini Uganda wakati wa hafla ya uzinduzi wa nembo na jezi za mashindano hayo kwa timu ya taifa hilo.
Tanzania, Uganda na Kenya ndizo nchi wenyeji wa mashindano hayo makubwa Afrika.
“Mashindano haya ni zaidi ya michezo kwakuwa yanajenga taswira yetu duniani, ni gurudumu la kusukuma fursa za kiuchumi na biashara,” amesema Museveni.
Pia amesema tangu aingie madarakani ameimarisha amani na huduma za elimu, na kwamba kwa sasa ni zamu ya michezo kwakuwa viwanja vimejengwa na juhudi zaidi zinaendelea kufanyika ili kukuza sekta hiyo.
Kiongozi huyo amesema mashindano ya CHAN yameipa Uganda changamoto chanya na shinikizo la maboresho zaidi ya miundombinu ya michezo.
“Tukiwa nchi washirika wa kuandaa mashindano haya na wenzetu Tanzania na Kenya, tunajivunia kuona yanaimarisha ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nazitakia kheri timu zote,” amesema Museveni.
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa mashindano ya CHAN, huku Kenya ikipewa nafasi ya kuandaa fainali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED