TIMU ya Tanzania ya Wanawake kutoka kituo cha Future Stars Academy cha jijini Arusha, imefanikiwa kushika nafasi ya pili katika michuano ya vijana wanaotoka kwenye mazingira magumu.
Michuano hiyo imefanyika kuanzia Agosti 22 hadi 30, 2025, jijini Oslo, Norway, yakishirikisha timu 60 kutoka mataifa 48.
Timu hiyo imefanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya kushinda mchezo wa fainali ya daraja la pili la michuano hiyo dhidi ya Austria kwa mabao 5-4.
Mabao yalifungwa na Loyce Dismas, Susan Michael, Varian Issa na Sarah Jacob.
Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza wa jumla kwa timu za wanawake alikuwa Uganda, baada ya kushinda mchezo wa fainali ya daraja la kwanza dhidi ya Romania.
Kenya, ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu, baada ya kushinda fainali dhidi ya Mexico, kwenye daraja la tatu la michuano hiyo.
Misri, ilichukua ubingwa wa jumla, huku Ureno ikishinda kwenye daraja la pili na Poland, kwenye daraja la tatu. Tanzania haikuwakilishwa na timu ya wanaume.
Balozi wa Tanzania anayewakilisha katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, Mobhare Matinyi, amewapongeza vijana hao kwa ushindi walioupata na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa walikuja wanne tu bila mchezaji wa akiba hata mmoja.
Mashindano haya huandaliwa kila mwaka na taasisi ya Homeless World Cup, yenye makao yake makuu nchini Uholanzi, ikishirikiana na shirika la Salvation Army.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu ya Tanzania kushiriki mashindano hayo, ambayo mwakani yatafanyikia nchini Mexico.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED