Zuhura ataja mwarobaini magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa wafanyakazi

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 10:02 AM Apr 27 2025
Zuhura ataja mwarobaini magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa wafanyakazi
Picha: Mpigapicha Wetu
Zuhura ataja mwarobaini magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa wafanyakazi

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Zuhura Yunus amesisitiza wafanyakazi wa sekta mbalimbali nchini kujenga tabia ya kushiriki michezo na kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanawakabili watu wengi ulimwenguni.

Zuhura alitoa wito huo wakati akifunga Bonanza la michezo (OSHA Bonanza) lililoandaliwa na kuratibiwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kama sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yaliyoadhimishwa kitaifa mkoani Singida katika Viwanja vya Mandewa.

 Zuhura alieleza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikihamasisha umuhimu wa michezo na mazoezi kwa wananchi ili kujenga afya na kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo saratani, kisukari, magonjwa ya moyo na shindikizo la damu.

“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinakadiria asilimia 75 ya vifo vyote vinavyotokea ulimwenguni kila mwaka husababishwa na magonjwa yasiyoyakuambukiza na hata Wizara ya Afya nichini inakadiria kati ya vifo 100 vinavyotokea kila mwaka vifo 33 vinasababishwa na magonjwa hayo, hivyo nawasishi wafanyakazi wote kuepuka mtindo mbaya wa maisha na kujenga tabia ya kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa haya” alieleza Zuhura


Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda alisema dhumuni kubwa la Bonanza hilo ni kutoa hamasa kwa wafanyakazi kushiriki michezo ili kujenga afya zao pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya wafanyakazi huku akieleza kuwa taasisi yake itaendelea kulinda nguvu kazi kupitia programu mbalimbali ikiwemo kaguzi za usalama na afya ili kuhakikisha wafanyakazi wote wanakua salama na wenye afya njema ili watekeleze majukumu yao vyema.

Bonanza hilo lilijumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu,mpira wa pete, mbio za magunia, riadha, mbio za vijiti, kuvuta kamba, kukimbiza kuku,mchezo wa kukimbia na ndimu na katika michezo hiyo OSHA imetwaa ubingwa katika michezo mchezo ya mpira wa pete, riadha kwa wanawake na wanaume huku timu ya mpira wa miguu ya OSHA Sports Club ikiishia hatua ya nusu fainali katika mchezo wa mpira wa miguu.


Aidha, timu zilizoshiriki katika michezo mbalimbali ya Bonanza hilo lililofanyika katika viwanja vya VETA Singida ni timu kutoka OSHA, Wizara ya ujenzi, Mgodi wa Geita (GGM),Wizara ya Uchukuzu, Mahakama, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji, Bohari ya Dawa (MSD),TANROADS,Shanta Gold Mine, Wizara ya Afya, Benki ya NMB, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikiali, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).