Madalali wadaiwa kuwalaghai wakulima wa dengu

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 07:32 AM Aug 23 2024
Zao la ndegu.
Picha: Mtandao
Zao la ndegu.

WAKULIMA wa dengu katika Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni Mkoa wa Singida wameiomba serikali kuwapa elimu ya mfumo wa stakabadhi gharani kufanya biashara kwa mnada na kuondokana na udanganyifu wanaodai kufanyiwa baadhi ya madalali mashambani.

 Wakizungumza na waandishi wa habari juzi kwa nyakati tofauti, walisema wametoa ombi hilo baada ya kubaini kuwa madalali wanaofika vijijini wanawapotosha kuhusu mfumo huo kwa lengo la kuwalangua mazao yao. 

Walisema madalali hao wamekuwa wakiwaeleza kuwa  wakipeleka mazao yao kuuza kwa mfumo huo watadhulumiwa fedha zao. 

Walisema madalali hao wamekuwa wakiwaambia kwamba kwa mfumo huo, huenda ikachukua hata miaka mitatu zaidi kulipwa fedha zao. 

Wakulima hao ambao walikuwa wakizungumza m katika ghara la Utemini Itigi linalotumika kukusanya na kuuzia dengu kwa njia ya stakabadhi gharani, walisema madalali wanaopita mtaani wananunua kwa bei kati ya Sh.1,300 hadi Sh.1,500 kwa kilo.

Walisema wasimamizi wa mfumo huo nao wamekuwa wakisema kwa minada mitatu iliofanyika mpaka sasa bei ya zao hilo haijashuka chini ya Sh. 1,900. 

Fidelis Mtoka, mkulima wa Kijiji cha Kazikazi Kata ya Kitalaka, alisema mpaka bado hajapata elimu ya kutosha juu ya mfumo huo na kubaki njia panda. 

“Kwangu bado mfumo sijauelewa vizuri, changamoto kubwa inayotupata sisi wakulima ni kuhusu bei, elimu haijatufikia,” alisema. 

Mkulima mwingine, Issa Abdalla, aliitaka serikali iwape elimu wakulima hususani vijijini ili waondokane na kauli za udanganyifu zinazotolewa na madalali hao. 

"Siku  ya kwanza nilipoambiwa kuhusu kupeleka mazao gharani nilipingana nao sana sababu sikuwa na elimu kuhusu mfumo ila baada ya kufuatilia nilielewa na nikajiunga," alisema. 

Abdallah, alisema hakuamini kama mfumo huo utakuwa kama anavyoshuhudia licha kuishauri serikali iwafikie zaidi wakulima hasa waishio nje ya mji.

Mwendesha ghala kuu kwa mfumo huo wa halmashauri ya Itigi na Manyoni, Remigeous Kailembo, alisema kadiri siku zinavyokwenda wakulima wanajitokeza zaidi kupeleka mazao yao gharani.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika na Masoko (AMCOS) Utemini Itigi, Geofrey Yohana, alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wakulima kwa kutumia magari kwa wakulima. 

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Itigi, Jonathan Dulle, alisema kama halmashauri mpaka sasa wamekusanya zaidi ya Sh. milioni 160 katika minada mitatu mwaka huu na hawajapokea malalamiko ya mkulima kutopokea hela ndani ya saa 48.