Mbaroni kwa kuchakachua gesi

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:23 AM Aug 23 2024
Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Lorivii Long’idu.
Picha: Mtandao
Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Lorivii Long’idu.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imewakamata wafanyabiashara watatu mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kuhujumu biashara ya gesi ya kupikia majumbani kwa kuchakachua ujazo na kuuza pungufu.

Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Lorivii Long’idu alisema kuwa, mitungi ya nishati safi ya gesi ya kupikia ni lazima ijazwe kwa kuzingatia uzito sahihi na kuuzwa kwa wateja. 

“Kwa Kanda ya Kaskazini, kuna idadi ya watu ambao tumewakamata kwa sababu kuna changamoto kubwa sana ya uchakachuaji. Kwa sababu eneo hili la Kilimanjaro lina barabara inayopeleka gesi nchi jirani ya Kenya,” alisema Long’idu wakati akitoa elimu kwa wadau wa gesi ya kupikia wa Manispaa ya Moshi na kuongeza kuwa: 

“ Kwa hiyo kuna uchakachuaji, hasa kwa haya magari makubwa yanayopita maeneo ya Himo, Holili . Kuna ile hali ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wanachakachua.” 

Alisema kwa kushirikiana na vyombo vya serikali, wamekuwa wakiwakamata, kuwafikisha mahakamani kujibu mashtaka.

 Alisisitiza kuwa mamlaka hiyo inaendelea na msako dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo hivyo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro ili kuwabaini wanaojihusisha na biashara hiyo bila ya  kufuata taratibu. 

Ofisa Vipimo wa Wakala wa Vipimo (WMA) Kilimanjaro, Yuda Thade, alisema makosa makubwa yanayotokea kwenye biashara ya gesi ni wauzaji au wafanyabiashara kutokuwa na mizani. 

Thade, alisema makosa hayo ni kuuza gesi ikiwa na uzito pungufu na kuuza gesi ambayo mtungi haujaandikwa.