Serikali yawapa bil. 6.8/- wananchi wahame hifadhini

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 08:40 AM Jan 01 2025
Fedha.
Picha:Mtandao
Fedha.

SERIKALI imetoa Sh. bilioni 6.8 kwa ajili ya fidia kwa wananchi wanaoishi katika kijiji cha Ngombo, wilayani Malinyi, mkoani Morogoro kilichomo ndani ya Pori la Akiba Kilombero ili wahamie maeneo mengine nje ya hifadhi hiyo.

Ofisa Maliasili Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa alisema hayo wilayani Malinyi jana wakati wa ufuatiliaji taratibu za wananchi kuhama maeneo yao na jinsi walivyoingiziwa fedha zao kwenye akaunti za simu zao ikiwa na kutatua changamoto ndogo kwao.

Chuwa alisema kuhamisha watu katika hifadhi hiyo kulianza miaka miatatu iliyopita kwa kuhamasha watu kupisha uhifadhi kupitia vikao mbalimbali hadi ngazi za chini.

"Katika kipindi hiki tupo kwenye kutekeleza zoezi hili na  linaendelea vizuri. Watu wana amani na wamejiandaa siku nyingi kwenda kuhamia sehemu ambayo wameichagua," alisema Chuwa.

Alisema wananchi wa kijiji cha Ngombo wanashukuru serikali kwa kuidhinisha fedha za fidia, kila mlengwa ameingiziwa katika akaunti yake kiwango anachostahiki.

"Wananchi wengi wao hawakuamini kama wangelipwa fidia na tena kwa haraka na tayari wameanza kubomoa nyumba zao na kuhama kwa hiari ili kuondoka kupisha uhifadhi kwenye eneo hili muhimu kwa shughuli za uhifadhi," alisema Chuwa.

Alisema eneo la kijiji cha Ngombo lenye ardhi oevu linategemewa kuongeza wingi wa maji katika Mto Rufiji ili kusaidia maji kuzalisha umeme katika Bwawa la Nyerere pamoja na kurudisha wanyama mbalimbali wakiwamo adimu.

"Katika eneo la hifadhi, wamo wanyama adimu ambao ni pamoja na sheshe ambao kwa asilimia 70 duniani wanapatikana Bonde hili la Kilombero," alisema Chuwa.

Alisema kijiji cha Ngombo kinapakana na mito mkubwa miwili ambayo ni Mpanga na Mnyera ambayo katikati yake ni kama kisiwa.

Chuwa alisema uamuzi wa serikali umewasaidia wananchi hao kuepuka nyakati za mafurukio ambayo yaliathiri robo ya kijiji na wakazi wake walilazimika kutumia mitumbwi, shule zilikuwa zinafungwa na kusababisha kuwapo mazingira hatarishi.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Jonas Makwati alisema kuwa eneo la Ngombo limo ndani ya Hifadhi ya Kilombero.

Makwati ambaye ni Kamanda Mhifadhi Nyanda za Juu Kusini wa mamlaka hiyo, alisema Hifadhi ya Kilombero ni pori jipya lililoanzishwa na serikali mwaka 2023.

Kamanda Mhifadhi wa Nyanza za Juu Kusini wa Mamlaka hiyo alisema kijiji hicho kimekuwa ndani ya  eneo la hifadhi ambapo kwa kujibu wa tangazo la serikali, wananchi wanapaswa kuwa nje ya hifadhi hiyo.

Makwati alisema zoezi litakapokamilika, wananchi wataondoka na wengine ambao wameshalipwa tayari wameanza kundoa baadhi ya mali ikiwa ni pamoja na kuezua mapaa ya majengo yao.

Mthamini Mteule wa Ardhi Mkoa wa Morogoro, Idelfonce Mtima alisema taratibu zote zimekamilika kuwezesha wananchi hao kuhama na kupisha eneo hilo.

Mtima alisema wananchi wanaofanyiwa uthamini ni 1,056 na waliohakikiwa na kustahiki kulipwa ni 807 na wengine zaidi ya 249 hawajakamilishiwa uhakiki na kwamba zoezi hilo linaendelea.

"Niwaombe tu wananchi kufuata taratibu, ambaye atakiuka taratibu za kuhama kwa siku ambazo zimepangwa atahama kwa gharama zake binafsi," alisisitiza Mtima.

Baadhi ya wananchi waliohakikiwa na kulipwa fidia kupisha eneo la kijiji hicho kwa nyakati tofauti walishukuru serikali kwa kulipa stahiki zao kwa muda unaotakiwa na wao wamekubali kuondoka kwa hiari.