TCB yaahidi kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo Zanzibar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:57 PM Aug 22 2024
TCB yaahidi kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo Zanzibar.
Picha:Mpigapicha Wetu
TCB yaahidi kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo Zanzibar.

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imeungana na wananchi wa kizimkazi Zanzibar, kwenye siku ya utalii kusherehekea ufahari wa utamaduni wa Kitanzania, vivutio vya utalii, umoja na mshikamano katika tamasha la Kizimkazi.

Benki hiyo imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, katika vipaumbele vyake vya kukuza maendeleo ya kiuchumi, kutengeneza ajira na kuwezesha ujumuishi katika kukuza uchumi wa buluu na upatikanaji wa huduma za kifedha visiwani humo.

Mkurugenzi  Mtendaji wa TCB,  Adam Mihayo, akizungumza leo visiwani humo, amebainisha dhamira ya TCB ya  kukuza maendeleo ya kiuchumi na uchumi jumuishi.

Amesema ni dhahiri katika kila jambo wanalolifanya kwasababu wanaelewa kuwa mfumo thabiti wa kifedha ni uti wa mgongo wa uchumi imara. 

Mihayo amesema Kama sehemu ya dhamira hiyo, imejizatiti kutumia fursa mbalimbali lengo likiwa kuboresha maendeleo ya kiuchumi ya Wazanzibar na  mojawapo ya mikakati hiyo ni mkataba wa makubaliano uliotiwa saini hivi karibuni baina ya benki na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA).

“Ushirikiano huu ni mpango wa utoaji wa mikopo inayolenga kuwanufaisha wanawake, vijana na makundi maalum wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi visiwani Zanzibar Lengo  kuu ikiwa ni kuvifikia vikundi 70, na tayari Sh. milioni 151 zimetolewa kati ya Sh. milioni 300 zilizotengwa kwa ajili ya kuwainua wajasiriamali,” amesema Mihayo. 

Mihayo amebainisha kuwa mpango huu unakusudia kuchochea ukuaji wa biashara, ongezeko la ajira, na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.

Mbali na mkakati huo, Benki ya TCB imejikita kuinua uchumi wa buluu hususani kilimo cha mwani.

 Ikitambua mchango mkubwa wa zao la mwani katika uchumi wa ndani, TCB imekusudia kuhakikisha kwamba wakulima hawa wanapata mikopo nafuu ili kufikia malengo yao.

Kwa kuwawezesha kiuchumi, TCB pia inawasaidia kuboresha maisha yao na kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa Zanzibar kwa ujumla.

Alisema kupitia programu na ushirikiano mbalimbali, wanakusudia kuimarisha uchumi na kujenga mazingira imara na rafiki kwa wote na wanabosherekea tamasha hilo na  kusherehekea pia kasi ya maendeleo ambayo kila mmoja ni mshiriki.