Wanawake, wasichana wawezeshwa kiuchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:39 AM Jan 01 2025
 Brac Maendeleo Tanzania
Picha:Mtandao
Brac Maendeleo Tanzania

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Brac Maendeleo Tanzania (BMT) limetumia Sh. 294,823,389 kuwawezesha wanawake na wasichana barehe kiuchumi wa Mkoa wa Singida kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Meneja wa shirika hilo wa mkoa huo, Isihaka Mirambo, aliyasema hayo wakati wa kukabidhi vifaa mbalimbali vikiwamo vyerahani kwa wanufaika. 

Mirambo, alisema shirika hilo lilitoa kiasi hicho cha fedha kupitia mradi wake wa Kuwawezesha Wanawake na Mabinti Barehe Kiuchumi (AIM) na kujikwamua na hali ngumu ya maisha kutokana na kukosa kipato. 

Alisema AIM ambao sasa umehitimishwa kwa Mkoa wa Singida ulikuwa ukitekelezwa katika Halmashauri za Wilaya ya Iramba, Manyoni na Manispaa ya Singida kuanzia Julai mwaka juzi. 

Alisema katika kipindi hicho shughuli zilizofanyika katika halmashauri hizo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali ya Mkoa wa Singida na halmashauri ni uwezeshwaji kijamii, kiuchumi na Uchechemuzi. 

Mirambo, alisema katika kipengele cha uwezeshaji kijamii, mradi huo ulilenga kutoa elimu juu ya masuala mtambuka ya kijamii ili kuwajengea uwezo wa kujiamini, kuchanganua na kutatua changamoto zinazowazunguka wasichana na wanawake.

 "Washiri katika kipengele hiki waliweza kupewa elimu juu ya masuala ya afya ya uzazi, athari zitokanazo na matumizi ya dawa za kulevya, mimba za utotoni , ujasiriamali na elimu ya fedha ambapo jumla ya wshiriki 3,787 walinufaika," alisema Mirambo.

 Alisema katika uwezeshaji huo wa kijami, vijana 72 wa kike na wa kiume walipata ajira ya muda kwa ajili ya kusaidia uwezeshaji. 

Mirambo aliongeza kuwa katika uwezeshaji kiuchumi. watu 1,429 wamenufaika, shughuli hiyo ililenga kuwawezesha wanawake na wasichana  kiuchumi kwa kuwapatia elimu na mafunzo, nyenzo ambazo wamechagua wenyewe katika sekta ya kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo.  

Alisema shirika hilo lilianzisha vikundi vya vikoba kama sehemu ya kuwawezesha wanawake na wasichana kiuchumi na kuwa na uwezo wa kujikimu katika hali ya dharura.

 Mirambo, alisema mpaka sasa vikundi 60 vilivyoanzishwa na kusajiliwa katika halimashauri husika na vina wanachama 983, akiba mpaka kufikia Novemba mwaka jana Sh.Milioni 91.5, mikopo iliyotolewa Sh. milioni 7.155 na wakopaji ni 239.

  BRAC Maendeleo limetoa mitungi ya gesi 179 ili kuunga mkono serikali kampeni yake ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuwawezesha wasichana na wanawake kujihusisha na biashara ndogondogo na kujipatia kipato.