Wanufaika TASAF wapewa miche parachichi

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 07:13 AM Aug 23 2024
Miche ya parachichi.
Picha: Mtandao
Miche ya parachichi.

WANUFAIKA 83 wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mtaa wa Kiumba Halmashauri ya Mji wa Makambako Mkoa wa Njombe wameishukuru serikali kwa kuwapatia miche ya parachichi.

Walitoa pongezi hizo juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka baada ya kutembelea kaya hizo.

Walisema baada ya miche hiyo ya parachichi kuanza kutoa matunda na kuuza kutawasaidia kubadilisha maisha yao na kukuza kipato chao.

Mmoja wa wanuafaika, Turafiona Kidenya alisema alipewa miche 10 na anamatumaini makubwa na mradi huo kwamba utawatoa kwenye umasikini.

Atuhididze Selemani alisema mradi huo ni mzuri na umekuja wakati sahihi kwa sababu miche hiyo ni ya kudumu na hivyo kuishukuru serikali kwa kuendelea kuwatunza.

Hivyo, aliiomba serikali kuwasaidia kupata maji ya uhakika ili kuweza kumwagilia miche hiyo wakati wa ukame.

Mratibu wa TASAF kutoka Halmashauri ya Mji wa Makambako, Neema Chaula alisema tatizo kubwa ambalo wameliona katika mradi huo ni ukosefu wa maji.

Hivyo aliahidi kulifanyia kazi ili walengwa hao waweze kufikia malengo ya kupunguza umasikini.

Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kiumba, Valentina Mgimba alisema Febuari mwaka 2023 walipokea miche 830 kutoka halmashauri kwa ajili ya kuwapatia walengwa wapatao 83 na kugharimu Sh. milioni 8.3.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka alisema mradi wa upandaji miti ya parachichi kwa wanufaika wa TASAF ni mradi unaogusa watu kwa sababu utasaidia kupata matunda na fedha.

Alisema: “Mimi nawaongeza kwa sababu mmekuwa mfano mzuri kwenye nchi, tumewapa miche 10 wengine mpaka 18 hadi 20 lakini mnaitunza vizuri na najua kuna shida ya maji tutaona namna ya kutatua”.