Wasiojulikana waiba kokoa mashambani, majumbani

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 05:07 PM Jul 01 2024
Zao la kokoa.
Picha:Mtandao
Zao la kokoa.

WATU wasiojulikana wanadaiwa kuvamia mashamba ya wakulima wa kokoa wilayani hapa Mkoa wa Mbeya, kuiba na kusababisha kupanda kwa bei ya zao hilo.

Bei ya zao hilo kwenye mnada wa mwisho ilipanda kutoka Sh. 6,000 kwa kilo moja mpaka Sh. 26,000.

Wimbi hilo la wizi wa kokoa linadaiwa kusababisha wakulima kulala mashambani usiku kulinda mazao yao yasiibiwe.

Vijiji vilivyopo  Kata za Itunge na Ndandalo ni miongoni mwa maeneo ambayo wakulima wa zao hilo wamekumbwa na wizi huo.

Mmoja wa wakulima hao wa Itunge, Ambakisye Mwotela, alidai wezi hao baada ya kubaini wakulima wanalala mashambani, wamebadili mbinu kwa kuanza kuvamia majumbani mwao nyakati za usiku na kuiba kokoa.

“Hali hii imekuwa hatari kwetu kwa sababu tunalazimika kulala mashambani, wezi hawa wanaweza wakatudhuru ama tukang’atwa  na nyoka, lakini kitendo cha wezi hawa kuanza kuja majumbani kinatutishia zaidi,” alilalamika Mwotela.

Yesebia Kodi, alidai wizi wa zao hilo umekuwa mkubwa zaidi baada ya soko  kuwa zuri kutokana na bei yake kupaa. 

 Kodi, alidai baadhi ya wezi hao wanachuma matunda mabichi, kuchemsha na kuchoma kwa moto na kuharibu ubora wa zao hilo.

“Hii yote ni kwa kuwa kipato ni cha juu, mtu anaona akipata lita mbili za kokoa anauza  mpaka Sh. 30,000, tunaomba serikali itusaidie kutoa elimu maana michezo mingine kama  hii inaharibu ubora wa zao letu,” alidai.

Ibrahim Mohamed, alidai  wezi hao wanapita mchana kwenye mashamba na kuweka alama kila tunda lililokomaa kisha kwenda kuiba usiku.

Alimuomba Mbunge wa Kyela, Ally Mlaghila kuwasaidia kuunda  vikundi vya ulinzi shirikishi katika kata za jimbo hilo ili  kudhibiti wizi huo.

Kwa upande wake,  Kinanasi aliahidi kuwawezesha vifaa kwa ajili ya vikundi vya ulinzi shirikishi na kuonya watu hao kuacha wizi huo kwa kutafuta kazi nyingine halali ya kujiingizia kipato.

“Nimezungumza na polisi wa Kata ya Itunge,  tumekubaliana kuanzisha klabu za ulinzi na walichoniomba ni vifaa kama makoti ya reflector, filimbi na tochi, ndani ya siku mbili nitatekeleza ili kazi ianze na wananchi msiibiwe tena,” alisema Mlaghila

Alisema kakao kwa sasa inauzwa Sh. 26,000 kwa kilo na kwamba atahakikisha anafanya kila njia kukomesha wizi huo na uharibifu wa zao hilo.