Trump:Si muhimu Zelensky kushiriki mazungumzo

By Enock Charles , Nipashe
Published at 07:24 PM Feb 22 2025
Rais wa Marekani, Donald Trump
PICHA:MTANDAO
Rais wa Marekani, Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump amesema hakuna haja ya kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelensky kushiriki katika mazungumzo ya kumaliza mzozo kati yake na Urusi.

Trump aliambia Redio ya Fox News kwamba Zelensky amekuwa akishiriki katika mazungumzo kwa miaka mitatu tangu uvamizi wa Urusi Februari 2022 na bado ameshindwa kumaliza mzozo huo.

"Kusema kweli, sidhani kama kuna umuhimu sana kwake kuwa kwenye mazungumzo," Trump alisema. 

"Wakati Zelensky aliposema kwamba hakualikwa kwenye mkutano (huko Riyadh), haikuwa kipaumbele kwa sababu amekuwa akifanya vibaya kwenye majadiliano."

Maoni ya Trump, kwa mujibu wa Bloomberg, yanamaanisha kuwa rais huyo wa Marekani ataendelea na mbinu yake ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Urusi. 

Alizungumza na Vladimir Putin kwa njia ya simu wiki iliyopita, na maofisa wakuu wa Marekani walikutana na wenzao wa Urusi nchini Saudi Arabia siku ya Jumatatu. Ukraine haikuwa katika mazugumzo ya Riyadh.