Msemaji wa Vuguvugu la M23, Lawrence Kanyuka, amekanusha madai ya Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) kwamba kulikuwa na mapigano wakati wa utwaliwaji wa Mji wa Bukavu.
Kupitia mtandao wa X, Kanyuka amesema taarifa ya OHCHR inapingana na hali halisi, akidai kuwa wanajeshi wa FARDC walitumia vibaya silaha walizotelekezwa na wazazi wao, hali iliyosababisha vifo vya watoto kabla ya kuingia kwa wapiganaji wa M23 mjini humo.
Februari 18, 2024, OHCHR ilieleza kuwa hali ya haki za binadamu Mashariki mwa DRC inazidi kuzorota, huku ikiripotiwa mauaji ya kiholela, ukatili wa kingono, na mashambulizi dhidi ya hospitali na maghala ya misaada ya kibinadamu.
Msemaji wa OHCHR, Ravina Shamdasani, alisema waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameongeza mgogoro wa kibinadamu na usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu, na kusababisha wimbi la watu kuhama. Alisema pia ofisi yao imethibitisha mauaji ya watoto yaliyofanywa na M23 mara baada ya kuingia Bukavu.
OHCHR imepokea taarifa za wanahabari, wanaharakati wa haki za binadamu, na wanachama wa mashirika ya kiraia kukabiliwa na vitisho. Aidha, kumekuwa na ukamatwaji wa kiholela na madai ya kurudishwa kwa nguvu kwa vijana wa DRC waliokimbilia nchi jirani.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa wafungwa waliotoroka gerezani wanatoa vitisho kwa waathirika na mashahidi wa kesi zao, jambo linalohatarisha usalama wa mawakili na watendaji wa sheria.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu, Volker Türk, ameitaka Rwanda na M23 kuhakikisha ulinzi wa raia katika maeneo wanayoyashikilia. Amehimiza pande zote kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kurejea kwenye mazungumzo ya amani kupitia michakato ya Luanda na Nairobi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED