KATIBU Mkuu wa Shirika la Nchi Wazalishaji wa Kahawa Afrika (IACO), Balozi Solomon Rutega, amesema maadhimisho ya Wiki ya Kahawa Afrika yamepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam wiki ijayo, ikiwa ni jitihada za kuendeleza zao hilo.
Ameyasema hayo leo Februari 21, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano wa Tatu wa Nchi zinazozalisha Kahawa Barani Afrika (G25).
Amesema IACO inaendelea kushirikiana na wadau wengine ikiwamo sekta binafsi kusaidia mkakati wa kuongeza thamani zao hilo.
Amesema mkakati mmojawapo ni kuanzishwa kwa shule za mafunzo ya ufundi wa kahawa na uundaji wa ajira katika minyororo ya thamani.
“Wiki ya Kahawa Afrika inayotarajiwa kuanza wiki ijayo jijini Dar es Salaam, ni moja ya mipango inayotoa fursa ya majadiliano yanayolenga kuongeza uratibu na ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi kati ya nchi zinazozalisha na kutumia kahawa na wadau wa kimataifa,” amesema Balozi Rutega.
Amesema Afrika ikiungana, inaweza kukabiliana na changamoto yoyote, kutengeneza fursa mpya na kujenga kesho yenye neema kwa bara lote la Afrika.
Kaulimbiu ya mkutano wa G25 ni ‘Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana kupitia Ufufuaji wa Sekta ya Kahawa Afrika’. Leo, mawaziri wa sekta ya kilimo wamekutana na kesho Februari 22, 2025 ni zamu ya Marais ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuhudhuria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED