Mji Mkuu Botswana wazingirwa na mafuriko

By Enock Charles , Nipashe
Published at 12:07 PM Feb 21 2025
Eneo kubwa la mji mkuu wa Botswana, Gaborone likiwa limefunikwa na maji.
PICHA:MTANDAO
Eneo kubwa la mji mkuu wa Botswana, Gaborone likiwa limefunikwa na maji.

Mafuriko makubwa katika mji mkuu wa Botswana, Gaborone yamesababisha shule na barabara kufungwa na maeneo mengi kuwa chini ya maji.

 Rais wa nchi hiyo Dumo Boko amesema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii kwamba mji mkuu unakabiliwa na athari mbaya ya mvua kubwa na mafuriko.

 “Leo nimetembelea maeneo yaliyoathirika kwa mafuriko, uharibifu wa miundombinu na makazi ya watu, ninatoa pole zangu za dhati kwa wahanga wa tukio hili” amesema Rais Boko.

Nyumba na biashara zimekumbwa na uharibifu mkubwa na watabiri wameonya kwamba mvua zaidi ya 50mm au zaidi inaweza kunyesha katika maeneo fulani katika saa 24 zijazo.

Serikali imesema jambo hilo huenda likasababisha mrundikano mkubwa wa maji katika maeneo ya mabondeni na kusababisha mafuriko na athari zaidi kwa miundombinu na mali.