Serikali yanadi utalii tiba kwenye mkutano wa kahawa

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:24 PM Feb 21 2025
Serikali yanadi utalii tiba 
kwenye mkutano 
wa kahawa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Serikali yanadi utalii tiba kwenye mkutano wa kahawa.

SERIKALI imeweka mkakati wa kuthibitisha huduma za matibabu ya kibingwa na bingwa bozezi, yanayotolewa nchini yathibitishwe na kutambuliwa kimataifa.


Wakizungumza na Nipashe leo Februari 21, 2025 pembezoni mwa Mkutano wa Kahawa barani Afrika (G25), Mratibu wa Utalii wa Matibabu katika Wizara ya Afya, Dk. Asha Mahita, amesema serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa pamoja na dawa na kusomesha wataalamu wa afya; kwa ajili ya kutoa huduma bora za kitabibu, ambazo zinaipa nchi sifa na hadhi ya kimataifa.

Amesema uwekezaji uliofanyika umeiweka Tanzania kwenye ramani ya matibabu barani Afrika, iliyovutia pia raia wa nje nyingine kuja kutibiwa; huku Tanzania ikipokea mialiko ya kwenda kuimarisha tiba kwenye baadhi ya nchi za Afrika.

“Mwezi huu tulipokea ujumbe kutoka nchi ya Burkina Faso, ambao walikuja katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ambao wanataka kujengewa uwezo katika matibabu ya moyo,” amesema.

Amesema kwa mwaka jana, Tanzania ilipokea wagonjwa 7,576 kutoka chi za Comoro, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Malawi, Zambia na Msumbiji, waliokuja kutibiwa.

Dk. Mahita ameongeza: “Kipekee tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuifungua nchi na uwekezaji mkubwa ambao umefanyika kwenye sekta ya afya. Huwezi kujitanza kama hujawekeza kwenye teknolojia kwenye afya, watumishi wenye weledi, dawa na utoaji wa huduma bora. Sisi kama nchi tumewekeza sana kwenye maeneo hayo yote.”

Kwa upande wake, bingwa wa magonjwa ya mapafu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Mwanaada Kilima, amesema mkutano huo ni fursa kwa Tanzania kuonesha huduma mbalimbali zilizopo zikiwamo za kibingwa.

“Muhimbili tunatoa huduma za kibingwa na kibobezi kama upandikizaji wa figo, upasuaji wa kisasa kwa kutumia tundu dogo, upasuaji rekebishi, upandikizaji wa mimba na huduma bingwa za uzazi. Lakini pia tuna huduma za kibobezi za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo ya mfumo wa hewa ambao haupatikani kwa urahisi katika nchi nyingi za Afrika,” amesema.

Kwa upande wake, bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk. Caroline Swai, amesema kwenye eneo hilo, Tanzania imejiimarisha kwenye uchunguzi na tiba, akitaja mashine ya PET-CT scan, inayoweza kubaini kwa haraka hatua ya ugonjwa kwa kila mgonjwa.

“Hii ni mashine ya kisasa kabisa inayotumika katika kutambua kwamba ugonjwa wa saratani uko katika hatua gani na inatoa mwanga kwa mtaalamu wa afya kupanga matibabu sahihi kulingana na hatua ya mgonjwa,” amesema.

Naye daktari bingwa wa upasuai wa matatizo ya Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dk. Zarina Shabhay, amesema taasisi hiyo imefunga vifaa vya kisasa vya matibabu, vikiwamo vinavyoweza kufanya upasuaji kwa njia ya matundu kwa usaidizi wa kamera maalumu.

“Tuna upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti, upasuaji kwa njia ya matundu bila kufungua kidonda. Tunafanya upasuaji mkubwa wa kurekebisha vibiongo; na kwenye mishipa ya fahamu, tunafanya upasuaji kutoa vivimbe vya mishipa ya damu bila kufungua fuvu,” amesema.