SERIKALI imezindua kampeni ya ‘SITAPELIKI’ mahsusi kutoa elimu kwa umma, ili kushughulikia masuala ya utapeli na ulaghai mitandaoni.
Kampeni hiyo imeanzishwa, ili kuongeza uwelewa kwa wananchi, kuhusu mbinu zinzazotumiwa na matapeli mtandaoni na kuwapa maarifa zaidi ya jinsi ya kujikinga na majaribio mbalimbali ya ulaghai na kujiepusha na udanganyifu wa mitandaoni.
Akizungumza katika kikao kazi cha serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano cha uzinduzi wa kampeni hiyo, kilichofanyika jijini Arusha, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amesema kampeni hiyo, inaenda kupambana na udanganyifu wa watu wachache, wenye malengo binafsi ya kurudisha nyuma maendeelo ya nchi.
“Kampeni hii ya ‘SITAPELIKI’ ina lengo la kutoa elimu kwa jamii, pamoja na kuchukua hatua maksusi, katika kushughulikia masuala ya kiutapeli na ulaghai wa mtandaoni,” amesema Waziri Silaa.
Silaa amekumbusha umuhimu wa kulinda taarifa binafsi, kwa kutaja jumbe sita ambazo zitaendelea kutumwa kwa watumiaji wote wa mtandao, ikiwamo ya kulinda taarifa zako, kwa kutumia nywila thabiti na toafauti kwa kila akaunti, zenye mchanganyiko wa maneno, namba, alama, herufi kubwa na ndogo pamoja na linda taarifa zako kwa kuogopa kubofya viunganishi (links) usivyo vifahamu.
Amesema kuwa bado Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi zingine za serikali, zinalinda na kuhakikisha usalama wa mtandao nchini. Huku akiongeza kuwa, haijawahi kutokea kesi ya kudukuliwa kwa taarifa za mtu pasipo mtu mwenyewe kutoa ushirikiano kwa wadukuzi ‘matapeli.’
“Hakuna kesi ya mtu yoyote, ambaye amedukuliwa kwenye mtandao, bila yeye kutoa ushirikiano ndio maana jumbe hizi sita, zinalenga kumtaka mtumiaji kuongeza umakini. Unapopata ujumbe, umeshinda bahati nasibu kadhaa, ingiza namba yako ya siri ama ingia kwenye link hii, anapo ingia ndio mwanzo wa utapeli.,” amesisitiza Silaa.
Aidha akizungumza pia katika ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla, amesema kikao kitaenda kujadili ‘Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali’ wa miaka 10, kuanzia 2024 hadi 2034, uliosainiwa na kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Julai 29, mwaka jana.
“Kwa kutambua umuhimu huo, wizara imeendelea kuweka jitihada mbalimbali na kuhakikisha, ina ratibu masuala ya kisera pamoja na kuweka mazingira wezeshi yatakayosababisha matokeo chanya ya utekelezaji wa pamoja wa mkakati wa uchumi wa kidijitali,” amsema Abdulla.
Hawwah Ibrahim Mbaye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mapema wakati wa kutoa salamu, amesema Serikali ya Zanzaibar, imendelea kuchukua hatua mbalimbali, ili kufikia malengo ya uchumi wa kidijitali, ikiwamo mradi wa ujenzi wa kituo cha uvumbuzi utakao jengwa maeneo ya Gwefumu.
Amesema kituo hicho, kinaenda kutoa mbegu za vijana waliolelewa, katika mafunzo ya uchumi wa kidijitali, huku akisisitiza kuwa taifa bado lina haja ya kuongeza wataalamu wa ulinzi wa kimtandao (Cyber Security), ili kuwapo na mapinduzi mazuri ya uchumi wa kidijitali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED