Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimeadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Programu ya Mwanamke Kiongozi (Female Future Program) sambamba na mahafali ya wahitimu wa awamu ya kumi ya programu hiyo.
Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Super Dome jijini Dar es Salaam, ikihudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, sekta binafsi, mabalozi, waandishi wa habari, na wadau mbalimbali wa ATE.
Mgeni rasmi wa tukio hilo alikuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye amehudhuria kwa mara ya tatu katika historia ya programu hiyo, tangu alipoizindua mwaka 2016 akiwa Makamu wa Rais. Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran, amemshukuru Rais kwa uongozi wake imara na mchango wake mkubwa katika kukuza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.
"Mhe. Rais, tunakushukuru kwa kuwa nasi tena leo. Tangu ulipozindua programu hii mwaka 2016 na kuhudhuria mahafali ya sita mwaka 2021, umeendelea kuwa mwanga wa matumaini kwa wanawake wengi wanaotamani kupaa katika nafasi za uongozi," amesema Ndomba-Doran.
Katika hotuba yake, Mtendaji Mkuu wa ATE ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia programu hii kwa muongo mmoja uliopita. Takwimu zinaonesha kuwa jumla ya wanawake 493 kutoka sekta binafsi na umma wamepata mafunzo haya, huku idadi ikiendelea kuongezeka. Aidha, kwa kutekeleza rai ya Rais Samia aliyoitoa mwaka 2021, ATE imetoa mafunzo haya kwa wabunge 150 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na kufanya jumla ya wanawake waliopitia programu hii kufikia 642.
Kwa upande wa matokeo chanya ya programu hii, Ndomba-Doran amebainisha kuwa wanawake 102 wamepanda katika nafasi za juu za uongozi, wengine 50 wamejiunga na bodi mbalimbali za maamuzi, na 6 wamepata nafasi za kuongoza taasisi tofauti.
"Mimi pia ni mmoja wa wahitimu wa awamu ya kwanza ya programu hii, na najivunia kuona mafanikio yake katika kubadilisha taswira ya uongozi wa wanawake nchini," amesema Ndomba-Doran.
Katika kuendeleza azma ya kuwawezesha wanawake katika uongozi, ATE imeanza mazungumzo na Jeshi la Polisi ili kuwajengea uwezo maafisa wanawake kupitia programu hii. Mtendaji Mkuu wa ATE amebainisha kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi tayari ameridhia mpango huo, na matarajio ni kupata msaada kutoka kwa Serikali ya Norway kupitia Shirikisho la Waajiri wa Norway (NHO) pamoja na washirika wa ESAMI.
Pia, ATE imeanzisha mtandao wa wahitimu wa programu unaoitwa Female Future Tanzania Network, ambao utasaidia wanawake waliopitia mafunzo haya kuendelea kushirikiana, kusaidiana, na kuimarisha ushawishi wao katika uongozi kwa kauli mbiu ya "Female Future Spirit – Making Each Other Better."
Katika hotuba yake, Ndomba-Doran amehitimisha kwa kuwapongeza wahitimu wa awamu ya 10 ya Programu ya Mwanamke Kiongozi na kuwashukuru wadhamini pamoja na wafanyakazi wa ATE kwa kufanikisha hafla hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED