Viongozi Makanisa Katoliki wakutana na M23, DRC yapiga ‘stop’ ndege za Rwanda

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 06:03 PM Feb 12 2025
Viongozi Makanisa Katoliki wakutana na M23, DRC yapiga ‘stop’ ndege za Rwanda.
Picha: Mtandao
Viongozi Makanisa Katoliki wakutana na M23, DRC yapiga ‘stop’ ndege za Rwanda.

VIONGOZI wa Makanisa Katoliki Nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENCO) pamoja na Kanisa la Kristo nchini humo (ECC), mapema leo Februari 12, 2025 wamekutana na kufanya mazungumzo na waasi wanamgambo wa AFC-M23 lengo likiwa ni kujadili udumishaji amani nchini humo.

Viongozi hao wamekutana na sehemu ya uongozi wa M23 katika Hoteli ya Serena mjini Goma ambako pamoja na mambo mengine wamewashukuru wanamgambo hao kwa kuendelea kudumisha amani katika mji huo walioutwaa hivi karibuni.

Wamesema kwa mara ya kwanza, Goma inafanya kazi saa 24 kwa siku, bila matukio ya wizi wa kutumia silaha au vurugu za aina yoyote tofauti na ilivyotarajiwa.

Vilevile kabla ya kikao hicho viongozi hao wanaelezwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa DRC Felix Tshisekedi.

Katika mwendelezo wa mzozo huo ambako serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaishutumu Rwanda kufadhili moja kwa moja mashambuli hayo mapema leo imefunga anga yake kwa ndege zote za kiraia na za serikali zilizosajiliwa au kutoka Rwanda.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Agence Congolaise de Presse ambako hata hivyo M23 wamehoji juu ya usitishwaji wa safari za ndege hizo kama ni mpango mkakati wa kiulinzi au mchezo tu wa kisiasa.

“Kuzuia ndege za Rwanda kutumia anga ya DRC huo ni ulinzi wa kimkakati au michezo wa kisiasa tu? Kukata ufikiaji wa anga hakutasuluhisha mizozo zaidi, Je, Kinshasa inafanya hatua ya ujasiri au inathibitisha tu kwamba haina washauri bora?,” wamehoji M23

Mamlaka ya uwanja wa ndege wa Kongo imetangaza katazo hilo ndani kuhusu marufuku rasmi ya kuruka na kutua katika eneo la DRC kwa ndege zote za kiraia na za serikali zilizosajiliwa nchini Rwanda au zile zilizosajiliwa kwingineko nchini Rwanda kutokana na hali ya ukosefu wa usalama iliyosababishwa na vita.

Takribani wanajeshi 20 wa kulinda amani wakiwemo 14 kutoka Afrika Kusini wameuawa wakati wa mapigano kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa Kongo. Mabaki ya wanajeshi hao wa Afrika Kusini yanatarajiwa kurejeshwa nyumbani siku ya Alhamisi.