Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura pamoja na kuboresha taarifa zao.
Zoezi hilo linatarajiwa kuanza kesho, Februari 13, na kumalizika Februari 19 mwaka huu.
Akizungumza katika kikao na wadau wa usafirishaji, viongozi wa dini na siasa, Dk. Burian alisema kuwa hata vijana wa miaka 17 waliobakisha miezi michache kufikisha umri wa kupiga kura wanapaswa kujisajili mapema.
"Kesho tunaanza zoezi la kujiandikisha, hivyo nawasihi wananchi wajitokeze kwa wingi. Pia, tutakuwa na uboreshaji wa taarifa na kampeni mbalimbali za kuhamasisha ushiriki wa wananchi," amesema.
Aidha, amewataka wananchi kujiandaa kwa mapokezi makubwa ya Rais Samia Suluhu Hassan, anayetarajiwa kuwasili mkoani humo Februari 23 kwa ziara ya kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED