MWANAFUNZI wa darasa la saba katika shule ya Msingi Lwemba, Kata ya Kidodi, wilayani Kilosa, John Kandole (11), amekamatwa na Polisi kwa kujaribu kumuua mama yake mzazi, Regina Kalinga (44), kwa kumuwekea sumu kwenye chakula.
Tukio hilo limetokea Februari 11, 2025 mchana katika kitongoji cha Msalabani juu, kijiji cha Iwemba, Kata ya Kidodi, Tarafa ya Mikumi, Wilaya ya Kipolisi Ruhembe-Kilosa, mkoani Morogoro,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amedai baada ya kijana huyo kuweka sumu aina ya Lara force, inayotumika kuua wadudu kwenye bustani ya mboga, kwa kuweka kwenye maharage yaliyopikwa na kuliwa pamoja na wali ambao ulipikwa na mama yake mzazi.
Akasema baada ya kula chakula mama huyo na watu wengine watano, walianza kuumwa tumbo na kukimbizwa hospital ya St. Kizito, na mama huyo akalazwa kwa matibabu zaidi.
Kamanda huyo wa Polisi amesema, watu wengine watano Eusebia Kamili (53), Zena Salehe (17), Patrick Ndola (11), Alvin Alex (5) na Hidaya Swedi (1) walitibiwa na kuruhusiwa.
Akasema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni mtoto huyo kuchukizwa na tabia ya mama yake ya kumtuma na kumpangia kazi nyingi, hivyo kumnyima muda wa kucheza na wenzake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED