DC Tarime asema bado wanamsaka Mwenyekiti wa CCM Kata ya Itiryo

By Ambrose Wantaigwa , Nipashe
Published at 03:33 PM Mar 13 2025
Mwenyekiti wa CCM Kàta ya Itiryo Wilaya ya Tarime, Peter Magahu
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa CCM Kàta ya Itiryo Wilaya ya Tarime, Peter Magahu

MKUU wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele, amesema vyombo vya ulinzi na usalama katika eneo hilo wanaendelea na oparesheni ya kumtafuta Mwenyekiti wa CCM kata ya Itiryo Peter Magahu akiwa hai au amefariki.

Mwenyekiti huyo anadaiwa kutekwa na watu wenye silaha waliojitambulisha kuwa polisi akiwa nyumbani kwake usiku wa Februari 9, 2025 na kuanzia siku hiyo juhudi za ndugu zake kumtafuta hazijafua dafu.

Kiongozi huyo amebainisha uwapo wa mawasiliano ya kiintelijensia na mkuu wa wilaya kutoka nchi jirani ya Kenya kutafuta uwezekano wa uhalifu wa mipakani kwa kuwa kata ya Itiryo, imepakana na nchi hiyo ya Afrika mashariki.

"Tumeenda mbali,tumewasiliana na DC(mkuu wa wilaya)ya Kenya,kuna vyombo vingine vinaendelea kufanya hii kazi, lakini tunahakikisha anapatikana akiwa hai au amefariki kazi ya serikali ni kuhakikisha inalinda usalama wenu(wananchi)

Katika hatua nyingine, Mkuu wa wilaya amepiga marufuku vyombo vingine vya usalama(hakuwataja) kufanya oparesheni bila kushirikiana na jeshi la polisi akiita ukamataji ovyo.

"Hakuna mtu atafanya hizi oparesheni bila kushirikiana na polisi,nataka niwaelekeze ma-OCD wote watatu wa Nyamwaga,Sirari na Tarime pasitokee tena ukamataji ovyo, kuwe na utulivu,taarifa ziwe za kweli tusisingiziane," alisema Kiongozi.

Mkuu wa Wilaya alikuwa anahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mpakani cha Itiryo wilaya ya Tarime, kilichoketi kujadili ulinzi na usalama kutokana na tukio hilo.

Awali, mara baada ya tukio hilo taarifa za kutekwa mwenyekiti huyo ziliripotiwa na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, nje ya ukumbi wa bunge, alitaja majina ya viongozi wengine wa CCM ngazi za kata mbalimbali wilayani Tarime kutishiwa.

Alihusianisha tukio hilo lililotokea katika kata yake ya asili anakotokea na wapinzani wake kisiasa (ambao hakuwataja) kuhujumu nafasi yake kuelekea uchaguzi mkuu ujao, kwamba wahanga wa matukio hayo ni wafuasi wake. 

Alieleza waandishi wa habari wakati huo kusikitishwa na mfululizo wa matukio ya kutekwa kiongozi huyo wa CCM kata wakati ambao pia kulikuwa na tukio la ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira.

Mkuu wa Polisi (OCD) wa eneo husika la Nyamwaga ASP Mohamed Mwadini, alisema wanatekeleza maazimio ya tume ya Rais ya haki jinai ikiwa pamoja na maelekezo kwamba taasisi yoyote isiendeshe ukamataji bila kushirikiana na polisi.

Kulingana na Anna Urio, mke wa Peter Magahu, watekaji walipofika nyumbani kwake usiku huo waligonga geti na kujitambulisha kuwa ni askari polisi huku wakiamuru wafunguliwe. 

Alisema Mume wake huyo aliwahoji kama wameambatana na kiongozi yoyote wa mtaa huo, ili awafungulie lakini kabla hajafungua walivunja geti na kuingia kisha wakavunja mlango wakaingia ndani.

Anaeleza kwamba watekaji hao walijitambulisha kuwa polisi wakagonga geti, Peter akauliza kama walikuwa wameambatana na viongozi wakamtishia kwa maneno, huku wakiendelea kuvunja geti.

"Ghafla geti likavunjwa wakaingia ndani, mume wangu akiwa sebuleni alikutana nao uso kwa uso,watu watano niliwaona mmoja akaanza kumshambulia (mume) kwa makofi akimtuhumu kwa mambo kadhaa ikiwemo kugoma kufungua mlango," alisema Anna.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walisema wanalazimika kutumia laini za simu za mitandao ya nchi jirani kutokana na uhaba wa mawasiliano hali inayosababisha kuchelewa kutoa taarifa za uhalifu.

"Kutokana na kukosekana network(mtandao wa simu)wafu wengi hapa wanalazimika kuvuka na kununua laini za simu za mitandao ya nchi jirani ili kutoa taarifa za uhalifu kwa muda muafaka"alisema Daudi Mwita mkazi wa Itiryo.

Alisema serikali iharakishe uchunguzi huo na haki ijulikane mapema kwa familia ya mwenyekiti huyo, aliyetekwa kwa kuwa inateseka kwa kukosa mahitaji ya msingi pamoja na msongo wa mawazo.