Fatma Ally: Ukondakta ni kazi halali, wasichana wapambane

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 05:58 PM Feb 19 2025
Mwanadada  Fatma Ally.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwanadada Fatma Ally.

Fatma Ally, binti anayefanya kazi katika magari ya Tilisho Safaris, amewataka wasichana kuachana na mtazamo hasi dhidi ya kazi ya ukondakta na kutambua kuwa ni kazi halali inayoweza kubadilisha maisha yao.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe Digital, Fatma amesisitiza kuwa kazi hiyo inampatia kipato cha kumudu maisha na kuendesha familia yake.

"Ukondakta ni kazi rasmi ambayo imerasimishwa na serikali. Kupitia kazi hii, nimekutana na watu mbalimbali wenye tija katika maisha yangu," amesema Fatma.

Fatma ameeleza kuwa jambo lililomvutia zaidi kuendelea na kazi hiyo ni namna inavyomsaidia kulipia mahitaji yake muhimu.

"Kazi hii inanifanya kuwa 'smart' muda wote, inanipa kipato cha kujikimu, na zaidi ya yote, ninajivunia kutoa huduma kwa jamii. Kuwahudumia abiria kunanifanya nihisi ubinadamu na upendo," ameongeza Fatma.

Fatma anafanya kazi kwenye magari yanayosafirisha abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha na Rombo, akihamasisha wasichana wengine kuchangamkia fursa za ajira badala ya kujifungia kwenye mitazamo hasi.