Rwanda yalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya waziri wake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:35 AM Feb 21 2025
Rwanda yalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya waziri wake.
Picha: Mtandao
Rwanda yalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya waziri wake.

Serikali ya Rwanda imelaani vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Waziri wake anayeshughulikia Muungano wa Kikanda, Jenerali Mstaafu James Kabarebe, ikimtuhumu kuhusika katika vita kati ya kundi la waasi la M23 na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mbali na Jenerali Kabarebe, Marekani pia imewawekea vikwazo msemaji wa kundi la M23, Lawrence Kanyuka. Rwanda imekuwa ikituhumiwa kwa kuunga mkono kundi hilo, lakini imeendelea kukanusha madai hayo.

Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, amesema kuwa vikwazo hivyo havina msingi wowote na ameitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za kisiasa za mataifa ya kikanda kutafuta suluhu badala ya kuchukua hatua alizozitaja kuwa "za kukatisha tamaa."

Makolo aliongeza kuwa vikwazo haviwezi kuwa suluhisho la mgogoro wa muda mrefu mashariki mwa DRC, akisema kuwa kama vikwazo vingekuwa na uwezo wa kutatua tatizo hilo, basi eneo hilo lingekuwa na amani kwa miaka mingi sasa.

Marekani ilitangaza vikwazo hivyo jana, ikimtuhumu Jenerali Kabarebe, ambaye kwa sasa ni Katibu wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda, kwa kuhusika na masuala ya ushirikiano wa kikanda.