NATHUBUTU kusema bila kigugumizi, kwamba Februari 5 mwaka huu
Dodoma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilifunika. Chama hicho kilifanya sherehe ya kukata na shoka katika kuadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwake.
Uwanja wa Jamhuri ulijaa na baadhi ya waliotaka kushuhudia wakashindwa kuingia, ikiwa ni kutokana na jinsi wahusika wa sherehe hizo walivyohamasisha wanachama na wasio wanachama, kufika kushuhudia kilichojiri.
Wanachama walikuwa na shauku ya kuona na kusikia ni nini kimefanywa na chama katika utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi 2020-2025, na pia kutaka kupongeza waliotangazwa wagombea urais wa Jamhuri na wa Zanzibar.
Lakini, upande wa wasio wanachama, walikuwa na shauku ya kuburudishwa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya kwa maana ya bongofleva, wacheza
ngoma, waimba kwaya na wasoma tenzi walivyokuwa wamejiandaa vilivyo kutoa burudani zao.
Hakika Dodoma ililifurika siku hiyo, kwa sherehe hizo kutanguliwa na mbio ndefu za marathoni, zilizovutia wengi sambamba na misafara ya baiskeli, pikipiki na mabasi mapya vyote vikiwa na rangi za chama hicho za kijani na njano.
Vituo karibu vyote vya redio na luninga, vilirusha matangazo mubashara, ili kuonesha Watanzania walioshindwa kufika Dodoma kushuhudia, kujionea kwa macho yao na kutambua jinsi CCM ilivyojiandaa kwa uchaguzi ujao.
Wakati watu wanajiuliza kwanini sherehe kubwa kama hiyo mwaka huu, wakati ingefanyika mwaka 2027 CCM ingekuwa imefikia Jubilei ya miaka 50 ambayo ni ya dhahabu,’ maswali hayo yaligusiwa pia na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyesema kweli kulikuwa na wazo hilo lakini mwaka huu ni muhimu.
Alikuwa akimaanisha, kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi, hivyo kama alivyosema pia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, sherehe hizo zilikuwa ni za kujaribu mitambo. Ni kweli CCM ilikuwa inafukiza sumu ya mbu chumbani, mbu wasisogee.
Kwamba inajua, vyama vya upinzani navyo vinajipanga kwa ajili ya uchaguzi na ndiyo sababu Mwenyekiti wa CCM.
Rais Samia Suluhu Hassan, akawahadharisha wanachama, kuacha kubweteka wakidhani wapinzani wamelala usingizi wa pono.
CCM katika maadhimisho hayo, ilijitahidi kuonesha misuli yake hususan ya kifedha, kwa kufanya maonesho ambayo ni dhahiri yalitumia fedha nyingi kwa maandalizi ya kwanza, kununua vyombo vipya kabisa vya usafiri kuanzia baiskeli mpaka mabasi ambayo ilielezwa vitagawanywa mikoani.
Pia, kuna kugharimia washiriki wa maadhimisho hayo kutoka mikoani, wakiwamo wasanii ambao hivi sasa wamegeuka kuwa nguzo kuu ya kuitangaza CCM na kuibeba katika masuala mbalimbali ya uhamasishaji wanachama.
Walishuhudiwa pia njiwa 500 waliorushwa uwanjani hapo kuashiria amani iliyopo, huku CCM ikijinasibisha kuisimamia na kuidumisha siku zote kabla, wakati na baada ya uchaguzi, lakini wote hao wakipatikana kwa fedha.
Kwa kurejea nyuma, ambako hakukuwahi kufanyika sherehe kubwa kama hizi, kwani wakati huo zikiishia kwenye matembezi ya mshikamano na hotuba za viongozi katika kila mkoa.
Pengine, hakutarajiwi kufanyika sherehe zingine kama hizi, labda pengine mpaka mwaka 2030, utakaokuwa wa uchaguzi.
Chama hiki kilionyesha misuli yake ya ukwasi, hasa kutokana na kufanya mkutano wake mkuu Januari 18 na 19 mwaka huu, ulioshirikisha washiriki wengi wakiwamo wajumbe, wasanii, wanahabari na wageni wengine waliogharimiwa kwa namna moja au nyingine.
Hata hivyo, imekuwapo hoja ya msingi miongoni mwa Watanzania, wakitaka kujua sababu ya chama hiki kufanya sherehe kubwa kama hiyo, ambayo ni ya maadhimisho ya kuzaliwa kwake, huku sherehe za kuzaliwa kwa taifa zikifunikwa.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, Rais John Magufuli, alizima shamrashamra za siku ya uhuru wa taifa hili, na badala yake fedha kupelekwa kwenye huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu.
Imekuwa hivyo hata enzi hizi za Rais Samia, kwa sababu ya kuchelea kufanya matumizi ya fedha kwa sherehe na kupelekwa kwenye huduma za kijamii.
Lakini jamii inajiuliza, ni kipi kikubwa kati ya siku ya kuzaliwa chama ambacho kinahusisha watu takriban milioni 12 na ya kuzaliwa taifa inayohusisha watiu takriban milioni 62.
Ni vizuri kuanzia mwaka huu, sherehe za uhuru ziadhimshwe kama zamani, kwa shamrashamra zaidi ya hata hizi za CCM, ili kuenzi siku tuliyoachana na minyororo ya wakoloni na kuwa huru, hatakuwezesha kuanzishwa vyama vya siasa kama vilivyopo sasa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED