Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV) zinapatikana bure kwa wagonjwa wote nchini.
Dk. Mollel alitoa kauli hiyo jana, Februari 20, 2025, wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya Mradi wa Timiza Malengo uliofanyika mkoani Lindi. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa maendeleo, huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Katika hotuba yake, Dk. Mollel alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu. Alifafanua kuwa zaidi ya shilingi bilioni 48 zimetumika kwa ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, na zahanati katika mkoa wa Lindi na maeneo mengine nchini.
Aidha, alibainisha kuwa huduma za kibingwa zinazojumuisha matibabu ya uvimbe wa ubongo bila upasuaji na matibabu ya saratani ya ubongo kwa kutumia teknolojia ya sauti maalum sasa zinapatikana nchini. Huduma hizi zilikuwa nadra kupatikana hapo awali, lakini sasa zimeimarika kutokana na jitihada za serikali.
Mradi wa Timiza Malengo awamu ya tatu unalenga kuboresha huduma za afya katika halmashauri 36 za mikoa 10 ya Tanzania Bara, ikiwemo Dodoma, Geita, Lindi, Mara, Morogoro, Njombe, Ruvuma, Singida, Tabora, na Tanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED