JWTZ, Mirembe wasaini mkataba utoaji huduma za afya ya akili

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 06:45 PM Jan 29 2025
JWTZ, Mirembe wasaini mkataba utoaji huduma za afya ya akili.
Picha:Mpigapicha Wetu
JWTZ, Mirembe wasaini mkataba utoaji huduma za afya ya akili.

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesaini Mkataba wa makubaliano ya Utoaji Huduma za Afya ya Akili na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa tiba kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  Brigedia Jenerali, Dk. Charles Mwanziva mara baada ya kusain Mkataba wa utoaji Huduma za Afya ya akili na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe.

Brigedia Jenerali Mwanziva amesema lengo kuu la mkataba huo ni kuwezesha wanajeshi wao kupata Huduma mbalimbali za afya zinazopatikana Hospitalini hapo.

“Mkataba huu utatusaidia sisi kama jeshi kupata Huduma mbalimbali zikiwemo Huduma za mazoezi ya viungo na Utengamao”, amesema Brigedia Jenerali Mwanziva

Amesema kuwa jeshi litafaidika kwa kiasi kikubwa katika Huduma za matibabu ya wagonjwa wa akili na hasa kwenye tiba maongezi (Huduma za kisaikolojia)

“Leo tumefahamu pia kuwa sio lazima kila mgonjwa anayekuja apewe dawa bali kuna tiba inaitwa ya maongezi ni tiba muhimu sana hasa kwetu wanajeshi itakayo mrudisha mtu katika hali yake ya kawaida pindi apatapo changamoto”, amesisitiza Brigedia Jenerali Mwanziva

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk. Paul Lawala amesema amefarijika kwa fursa ya JWTZ kushirikiana kwa karibu katika kutoa Huduma za kibingwa na bingwa bobezi katika eneo la afya ya akili.

“Napenda kulipongeza jeshi kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na sisi namna ya kuhudumia watu wao lengo ikiwa ni kuboresha ufanisi na utendaji kazi wa jeshi kwa kuhakikisha watumishi wao wanakuwa imara katika afya zao za akili”, amesema Dk. Lawala.

Dk. Lawala amesema kuwa mahitaji ya huduma ya afya ya akili katika jamii ni makubwa sana hivyo tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kusaidia jamii kuwa na uelewa juu ya magonjwa ya akili na dhana pana ya afya ya Akili.