KIPIGO WANAFUNZI; Mufti Mkuu aonya walimu madrasa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:21 PM Feb 19 2025
Mufti Mkuu wa Zanzibar
Picha: Mtandao
Mufti Mkuu wa Zanzibar

OFISI ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, imesema imepokea kwa masikitiko taarifa iliyoenea mitandaoni, ikimuonesha mwalimu wa madrasa, akiwaadabisha wanafunzi katika hali isiyo ya kawaida.

Imesema baada ya tukio hilo,e kufuatilia taarifa hiyo imebaini kuwa mhusika ni mwalimu wa madrasa katika Masjid Sunna kwenye msikiti uliopo Mbagala kwa Nyoka, Dar es Salaam.

Kadhalika, tayari taarifa hiyo imefikishwa katika Kituo cha Polis! Maturubai, Mbagala Kizuiani, kwa hatua za kisheria.

Kutokana na tukio hilo, Ofisi ya Mufti Mkuu, inawaasa na kuwasihi walimu wote wa madrasa kuwa waangalifu wakati wa kuwaadabisha wanafunzi na kujiepusha na matumizi ya adabu za kuumiza mwili.

Pia hali hiyo itawajengea mapenzi wanafunzi hao katika kuisoma elimu ya dini ya kislamu, kadhalika kujiunga na mafunzo ya ualimu kwa walimu wa madrasa yanayoendelea kutolewa nchini.

Imesema inaunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kuweka mikakati na mazingira bora ya kutunza na kuwathamini walimu wa madrasa.

“Wazazi na walezi waendelee kutoa ushirikiano ya karibu kwa walimu wa madrasa juu ya maendeleo ya watoto wao na kuwa karibu kufuatilia mwenendo mzima wa nidhamu na maadili ya watoto katika madrasa.”