WANANCHI wa Kishapu,wameelezwa kukosa huduma ya majisafi na salama kwa muda wa siku 10 sasa, hali ambayo inahatarisha Afya zao kwa kupatwa na magonjwa ya mlipuko ukiwamo kipindupindu hasa katika msimu huu wa mvua, huku kata mbili za Ngofila na Masanga zikipatwa na ugonjwa huo.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 6,2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wilayani Kishapu.
Diwani wa Kishapu Joel Ndettoson,ambaye ni mwakilishi wa wananchi, amesema sasa hivi kuna shida kubwa ya majisafi na salama wilayani Kishapu, ambapo mabomba hayatoi maji tena.
"Hapa Kishapu kuna "Crisis" kubwa sana ya maji, zimefika siku 10 sasa mabomba hayatoi maji,na tatizo hili limegusa Kata 5," amesema Ndettoson.
Meneja Wakala wa Maji safi na usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)wilaya ya Kishapu Mhandisi Dickson Kamazima, amekiri kweli tatizo la kukatika kwa maji lipo,na kubainisha kwamba shida ipo kwa Kashwasa,kwamba bomba la kupeleka maji wilayani humo kuna presha inasumbua kilomita moja na kusababisha mabomba kupasuka.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, amesema kutokana na ukosefu wa maji wilayani humo, sababu ya bomba kuu la kupeleka maji kupasuka,alikutana na Katibu Tawala wa Mkoa ili kutoa msukumo wa ukarabati wa bomba hilo, na kwamba jitihada zimefanyika ili kurejesha huduma hiyo ya maji.
Aidha,amesema ataunda timu ili kufanya uchunguzi wa kudhibiti tatizo la kupasuka kwa bomba la maji mara kwa mara tena eneo hilo hilo,na kusababisha wananchi kukosa huduma ya maji.
Ametoa pia tahadhari kwa wananchi, kwamba wazingatie kanuni za Afya ikiwamo kuchimba vyoo pamoja na kuvitumia, ili kukabiliana na mlipuko wa Kipindupindu, ambapo tayari Kata mbili za Ngofila na Masanga zimeshakumbwa na Kipindupindu, lakini tatizo hilo wamekabiliana nalo na ugonjwa huo umeisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED