TRA kutoa elimu ya kodi kwa viongozi wa dini nchini

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 04:00 PM Jan 02 2025
TRA kutoa elimu ya kodi  kwa viongozi wa dini  nchini.
Picha: Mpigapicha Wetu
TRA kutoa elimu ya kodi kwa viongozi wa dini nchini.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imepanga kutoa elimu ya kodi kwa viongozi wa dini zote nchini, ili waweze kuwaelimisha waumini wao kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, hatua inayolenga kuchochea maendeleo ya taifa.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, ametoa kauli hiyo leo, Januari 2, jijini Dar es Salaam, wakati alipokutana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk. Abubakar Zubeir, katika ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) zilizopo Kinondoni.

Akiwa ofisini hapo, Mwenda amempongeza Mufti Dk. Zubeir kwa juhudi zake katika kutoa elimu ya kodi kwa waumini na kuhakikisha taasisi za kidini chini ya BAKWATA zinalipa kodi ipasavyo.

“Licha ya BAKWATA kuwa taasisi ya kidini, mnajihusisha na shughuli mbalimbali ambazo zinawajibisha ulipaji kodi. Tunawapongeza kwa mfano mzuri mnaotoa,” amesema Mwenda.

Mwenda amesisitiza kuwa kulipa kodi ni ibada, na taasisi za kidini zina nafasi kubwa ya kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa waumini wao.

“Waumini wa taasisi za kidini wanawajibika kulipa kodi. Tunawahakikishia kuwa TRA itatenda haki kwa kila mtu. Anayestahili kulipa kodi atalipa, lakini hatutamuonea asiye na wajibu huo,” ameongeza.

Amebainisha kuwa kutumia majukwaa ya kidini kufikisha elimu ya kodi ni mkakati muhimu kwa kuwa viongozi wa dini wana ushawishi mkubwa kwa waumini wao.

“Faida za kodi ni nyingi. Leo hii watu wanapata matibabu, watoto wanasoma, na nchi inajengwa kupitia kodi. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuchangia maendeleo haya,” amesema Mwenda.

Ili kufanikisha mpango huo, Mwenda amesema kuwa timu ya wataalamu wa TRA kwa kushirikiana na BAKWATA itatengeneza mpangokazi wa pamoja. Mara utakapokamilika, utekelezaji utaanza mara moja.

Kwa upande wake, Mufti Dk. Abubakar Zubeir ameishukuru TRA kwa kufika ofisini kwake, kuwapongeza, na kujadiliana kuhusu njia bora za kupanua wigo wa ulipaji kodi.

“Ni muhimu viongozi wa dini kupata elimu ya kina kuhusu kodi. Hii itatusaidia kueleza waumini wetu kwa usahihi umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa,” amesema Mufti Zubeir.