W’biashara watoa kilio upatikanaji Dola

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:46 AM Jan 04 2025
Dola ya Kimarekani.
Picha:Mtandao
Dola ya Kimarekani.

WAFANYABIASHARA wanaonunua bidhaa nje ya nchi wamesema licha ya Dola ya Kimarekani kushuka thamani dhidi ya Shilingi ya kitanzania, upatikanaji wake umeendelea kuwa wa shida na kuwasababishia usumbufu wa kuitafuta hali inayowafanya kuingia hasara kibiashara.

Mapema mwaka 2023, nchi ilikumbwa na uhaba wa Dola nchini uliotokana na kuadimika kwa fedha hiyo katika Soko la Dunia, sababu kuu ikielezwa kuwa ni athari za ugonjwa wa UVIKO 19 ulioikumba ulimwengu tangu mwaka 2019 na vita vya Ukraine na Urusi.

Kuadimika kwa fedha hiyo kulisababisha usumbufu kwa wafanyabiashara nchini hasa wanaoagiza bidhaa nje ya nchi kwa kuwa walilazimika kuinunua kwa gharama kubwa hadi Sh. 2,800 kutoka kwa watu binafsi baada ya kukosekana benki.

Hata hivyo, serikali ilifanya juhudi kuimarisha sarafu ikiwamo kuunda kikosi kazi cha wataalamu kilichotafiti hali hiyo na kushauri hatua za kuchukuliwa na kadri siku zilivyosogea dola ilikuwa ikishuka thamani dhidi ya shilingi ya kitanzania.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, juzi fedha hiyo iliuzwa kwa Sh. 2,406 kutoka Sh. 2,700 bei ya Oktoba, mwaka jana, hali iliyokuwa ikisababisha hasara kwa wafanyabiashara nchini.

Mfanyabiashara wa nguo za kike Kariakoo, Ramadhani Ngang’uli alisema walitegemea baada ya dola kushuka thamani ingepatikana kwa urahisi kama ilivyokuwa mwanzo, lakini mambo yamekuwa tofauti.

Alisema wanapokwenda kununua fedha hiyo kwenye benki, wanaikosa na kuendelea na utaratibu wao wa kuitafuta kutoka kwa watu binafsi ambao huwauzia kwa bei ya juu ukilinganishwa na wanayonunulia benki.

Alisema wanalazimika kuitafuta fedha hiyo ili kupunguza gharama za kuagiza mzigo kutokana na baadhi ya mawakala wa usafirishaji kutumia fursa hiyo kuwauzia fedha hiyo kwa bei ya juu.

“Yaani ni kwamba mawakala wa usafirishaji wa mizigo wameshajiwekea utaratibu wao wa kulipia kwa dola kwa hiyo kama huna dola wao ndio wanakupangia ‘exchange rate’ (gharama za kubadilisha fedha) ambayo ni kubwa kuliko benki au mitaani,” alisema.

Mfanyabiashara Lemsi Mazengo, alisema japokuwa upatikanaji wa dola umeimarika kwenye benki, lakini hautimizi haja za wafanyabiashara, akitoa mfano kuwa kwa sasa wanaweza kuuza hadi dola 500 tofauti na hapo awali walikuwa wanauza dola 100 pekee kwa kila mteja tena kwa masharti.

Alitaja moja ya masharti hayo kuwa ili uuziwe fedha hiyo katika benki ni lazima uwe mteja wao wa kila siku uliyefungua akaunti hali iliyokuwa inaleta usumbufu na baadhi kuuziwa 100 pekee kwa siku.

Alisema hata hivyo, bado fedha hiyo imekuwa ikipanda na kushuka akitoa mfano kuwa juzi ilikuwa ikiuzwa Sh. 2,406, lakini jana iliuzwa kwa Sh. 2,500 hali inayoashiria kuwa bado tatizo hilo halijakaa sawa.

Alisema hali hiyo pamoja na kuleta usumbufu wa kuitafuta pia wakati mwingine inasababisha hasara, kwa kuwa wanaweza kununua mzigo wakati dola ipo juu, lakini mzigo unaofika na kuanza kuuza, dola inakuwa imeshuka na kulazimika kuuza bei ya chini.

“Unaweza ukanunua mzigo kwa dola ikiwa juu, lakini ikishuka itakulazimu uuze kwa bei ndogo kutokana na kushuka kwake kwa hiyo wakati mwingine unaweza kupata hasara kabisa,” alisema Mazengo. 

Mfanyabiashara Jabiri Mtoro, alisema, anatambua kama dola imeshuka, lakini yeye anaipata kirahisi kwa sababu ananunua kwa watu binafsi badala ya kwenda benki.

Mfanyakazi wa Benki ya Akiba Commercial (jina tunalihifadhi), alisema upatikanaji fedha kwa sasa umeimarika kuliko zamani na kufikia hatua ya kuuza hadi dola 5000 kwa siku tofauti na miezi sita iliyopita walikuwa wakitoa dola 1000 pekee.

Alisema kinacho sababisha dola kuadimika ni baadhi ya wafanyabishara wakubwa hasa katika sekta ya utalii ambao ndio wanaopokea dola kwa wingi kutozipeleka benki na kuziuza wenyewe mitaani.

Alisema hali hiyo inasababisha benki kukosa fedha za kuuzia wateja kwa sababu wanategemea kupata kutoka kwenye makundi hayo na si Benki Kuu kama wengi wanavyofikiri.

“Hii imekuwa biashara kwa sasa ikishuka wenye mitaji mikubwa wananunua, wanahifadhi wanategemea ikipanda na wao wanauza kwa hiyo tabia hiyo inafanya mzunguko wa dola kuwa mdogo hata kama imeshuka,” alisema.

Kadhalika, hali hiyo imekuwa tishio pia kwa wafanyabiashara na wengine wanaogopa kununua bidhaa za gharama kubwa kutokana na kupanda na kushuka kwa fedha hiyo.

BoT YAFAFANUA

Ofisa Habari Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Victoria Msina, amesema benki hiyo ilitoa miongozo kwa miamala ya kifedha nchini ifanywe kwa shilingi ya kitanzania na si dola ili kuwaondolea usumbufu na hasara wafanyabiashara.

Amesema hata taarifa mbalimbali wanazozitoa kwa umma kupitia tovuti yao wanahamasisha kutumia Shilingi za Tanzania na kwa sasa inaonekana imepanda thamani ikilinganishwa na Dola ya Marekani.

“Ndio maana serikali inasisitiza wananchi wafanye miamala mbalimbali kutumia fedha zetu hata shule za ‘international’ wanashauriwa walipe ada kwa kutumia fedha za Tanzania.