HERI ya Mwaka Mpya msomaji wangu. Tumshukuru sana Mungu kwa uhai huu aliotukarimu kwa upendo wake mwingi. Tunaendelea kumulika anga la wanaume.
Makala ya mwisho mwaka jana, tulianza kuangalia mambo ya msingi wanayopaswa kuzingatia wanaume katika nafasi zao kama baba wa familia.
Nikasema kuna kitu kikubwa sana Mungu anatarajia kwa kina baba. Mungu ana wathamini, hivyo msimwangushe. Mungu alimuumba mwanamume kwa kumwamini. Alimpa nafasi ya kwanza kupokea pumzi!
Hiyo ilikuwa nafasi ya kipekee kwa mwanamume. Hata siku moja usijute eti kwa nini Mungu alikuumba mwanamume, alikuthamini. Alikuumba kwa kusudi maalumu.
Baada ya kumuumba alimpa kazi/majukumu kwenye bustani ya Eden. Aliyepewa kazi na maelekezo ni mwanamume. Kwa mantiki hiyo, mwanamume usioe kabla ya kazi utakwama.
Naam, ili sasa mwanamume huyu asimwangushe Mungu nilitaja baadhi ya mambo ya msingi ya kuzingatia; kuwa mstari wa mbele kwa mambo ya Mungu. Hapaswi kuwa mbali na Mungu.
Kingine nikataja ahakikishe anafanya kazi kwa bidii. Kabla ya mwanamke Mungu alimpa mwanamume kazi. Wanawake wamekuwa chanzo cha wanaume kuathiriwa ndani ya ndoa.
Leo twende zaidi kumtahadharisha mwanamume awapo katika ndoa yake. Usikubali kulishwa na mwanamke kwani ataishia kukudharau. Siku ukila chakula cha mwanamke ambacho hujakitolea fedha ya matumizi, kimbia!
Unaweza kujikuta yupo mwanamume nyuma yako, ipo picha ya mwanamume mwingine, ndiye anatoa matumizi nyumbani kwako. Usikubali kula chakula cha bure. Wanawake hawajaumbiwa kutoa bali kupokea!
Mwanamke ukitaka kupata fedha toka kwa baba (mume), tumia mbinu. Na mwanamke akitoka afanye kazi na asirudi nyumbani mikono mitupu. Mwanamke aneyejitambua harudi nyumbani mikono mitupu.
Pointi nyingine ili mwanamume asimwangushe Mungu, hakikisha unalima. Wapo baadhi ya wanaume huwaachia wanawake kazi zote. Kazi nyingine ya mwanamume ni kutunza/kulinda.
Hakikisha mnawalinda wote walio chini yenu. Mengi yanatokea kwenye familia, kisa baba hawatambui jukumu lao. Kwa mfano, mwanamume akiomba heshima kwa mkewe, kuna shida kwani heshima haiombwi!
Mwanamke anapohisi kushambuliwa hutoa sumu zote mwilini. Mwanamke anapohisi halindwi aweza kuwa chochote. Kazi ya kuatamia ni ya baba!
Wanawake kwa asili wana wivu wanapohisi kuna mtu anaingilia anga lao. Na mwanamke akianza kulipa kisasi, hata shetani hukaa pembeni anachukua taarifa.
Linda mke wako, usiruhusu mume aungane na ndugu zake kumshambulia mke. Linda familia yako! Unaweza kumhudumia mke wako unavyotaka wewe kwani huyo ni wako.
Mwanamke huhamisha moyo. Unaweza kufikiri una mke kumbe alishahama. Humsemeshi mwenzio wiki nzima, akipata kidumu nje utakoma. Yaliyowakuta wanalifahamu hilo.
Mungu katika neno lake anaagiza; Enyi wake watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu (Waefeso 5:22). Kwa asili mwanamke anatii pale anapoona kitu.
Wapo ambao hawatii waume zao kama baba zao wa kiroho. Wanawake wanapaswa kupunguza jeuri kwani mume ni kichwa cha mkewe.
Mtu aweza kujiuliza; kwa nini wanawake hawana utii kwa waume zao? Jibu ni kuwa hawana upendo. Ukweli ni kwamba tunahitajiana, kila mmoja akifanya sehemu yake kila kitu kitakwenda sawa.
Neno la Mungu linatoa angalizo kuwa; 1Petro 3:7 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu. maombi yenu yasije kuzuiliwa”.
Mwite jambo linapotokea, badala ya kutulia, unakasirika. Unapokosea usitumie ubabe, eti mimi ni mwanamume. Nyuma ya kila mwanamume aliyefanikiwa yupo mwanamke aliyesimama. Hali kadhalika katika kuanguka.
Mwanamume usimfanye mwanamke agumie maumivu ndani ya moyo. Ishi na mwanamke kwa akili, maombi yako yasije kuzuiliwa. Kama hukumlinda akawa na sumu ndani, analia huwezi kupenya!
Wanawake wengi wamekandamizwa na waume zao. Usimlinganishe mume wa mwenzio na yule wa kwako kwani uwezo unatofautiana.
Usimseme mkeo kwa watu, mlinde asijue. Makahaba wengi wanamshambulia mke kwa kuwa mwanamume amewapa nguvu. Anamchokoza yule aliyemlipia mahari.
Mwanamke anamwambia mume hao wanawake zako waambie waache kunishambulia. Lakini bado anapuuzia kwa kuwa amewapa nguvu na kuwa karibu nao kuliko mke.
Kingine mfundishe mkeo. Wakati Mungu anampa Adamu maelekezo, mwanamke hakuwapo. Usimseme kwa watu, usimtolee mifano.
Hakuna familia iliyokamilika, elewa kinachomsibu mwenzako, usimsemeseme. Kinachotokea kwenye familia msikiseme.
Je, una maoni? Ujumbe 0715268581
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED