MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema atawatuma kwa siri watu aliowaita ‘mashushu’ kuwachunguza wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu wa msingi, ambao wataukanyaga mwongozo wa kitaifa wa ubainishaji na upimaji wa watoto/wanafunzi wenye mahitaji maalum ya elimu.
Amesema anataka kujiridhisha kuhusu jambo hilo, akisisitiza hataki mzaha katika mapokezi ya wanafunzi wenye ulemavu, kwa kuwa serikali imeweka miundominu rafiki kwa watoto hao.
Alidokeza kuhusu mpango wake wa kusimama na wenye ulemavu kupata haki ya kielimu, baada ya kukagua miradi ya ujenzi na ukarabati wa shule sita zilizoko Wilaya za Siha, Hai na Moshi, juzi.
“Tutafanya utaratibu na TAMISEMI (Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), kuona namna ya kupata walimu watakaosaidia hasa katika zile shule mpya zitakazopokea wenye mahitaji maalum. Kilimanjaro, tumejipanga kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bora.
"Nitatuma watu wangu kimya kimya wanipigie picha na kama hamjamaliza tutaelewana vibaya."
Mwongozo wa kitaifa wa ubainishaji na upimaji wa watoto/wanafunzi wenye mahitaji maalumu ya kielimu wa mwaka 2023 na Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi (MKEJ), unaelekeza kuwa utoaji wa elimu kwa wote bila ubaguzi, utachangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa Taifa la Tanzania, ambayo ni ya haki, usawa na ujumuishi.
Aidha, aliwataka wazazi/walezi wenye changamoto ya ukuaji wa kiakili na kimwili, kutowaficha ndani watoto hao, badala yake wapelekwe shule ili wapate elimu.
Akizungumzia tabia iliyojengeka katika jamii ya kuficha watoto wenye mahitaji maalum, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la TUSONGE CDO linalofanya kazi na jamii ya wenye ulemavu, Aginatha Rutazaa alisema:
“Jamii imekuwa ikiwaficha ndani wasionekane, lakini kumbe ndani wana utajiri mkubwa, wakitoka nje kufundishwa na kushirikiana na wengine wataleta furaha, ambayo Tanzania na ulimwengu unaitafuta katika fedha na mambo mengine.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED