Wapinzani waendelea kutimkia CCM

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 09:46 AM Jan 04 2025
   Wapinzani waendelea kutimkia CCM.
Picha:Shaban Njia
Wapinzani waendelea kutimkia CCM.

WANACHAMA 24 wakiwamo viongozi wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ushetu wilayani Kahama, mkoani Shinyanga wamehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai kuwa serikali imetekeleza malalamiko yao.

Makada hao ambao kati yao 18 wanatokea CHADEMA, moja ni NCCR-Mageuzi na watano ni kutoka TLP, walifikia uamuzi huo juzi baada ya mkutano wa hadhara wa Mbunge wa jimbo hilo uliolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi.

Mmoja wa makada hao ambaye ni Katibu wa Baraza la Wazee CHADEMA, Jimbo la Ushetu, Emmanuel Machibya, alisema hatua ya serikali kupelekea maendeleo wananchi hasa kwenye sekta ya afya, elimu na maji imewafanya kukosa cha kusema wala kukosoa.

Alisema hiyo ndio sababu kubwa iliyofanya kuachana na vyama vyao na kujiunga na CCM ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Alisema, miongoni mwa vitu walivyokuwa wakivisemea sana na vimetekelezwa ni pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Ushetu na utekelezaji wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria, ambao unakaribia kuwafikia.

“Tunatumia maji ya kwenye visima tulivyochimba wenyewe na vile vilivyochimbwa na RUWASA, na maji ya Ziwa Victoria, tulikuwa tunayatumia pale tunapofika Halmashauri za Msalala na Manispaa ya Kahama na sasa yanakuja kwetu hivyo hatuna haja ya kuendelea kupiga kelele huku miradi inatekelezwa na serikali,” alisema Machibya.

1

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), Kata ya Kisuke, Kulwa Chanila alisema, katika mradi wa maji wa Ziwa Victoria, vijana wamepewa ajira zisizohitaji ujuzi za uchimbaji wa mitaro ya bomba, kusogeza bomba nyinginezo na wanajipatia fedha za kuendesha maisha yao na hakuna ubaguzi uliofanywa wa kuwatenga vyama vya upinzani.

Alisema, kitu kingine kilichomvutia ni uwapo wa huduma bora katika vituo vya afya wakati wa kujifungua kulinganisha na awali.

Akipokea wanachama hao wapya, Mbunge Cherehani aliwaahidi kuwapatia ushirikiano na kuendelea kuwahudumiwa wananchi pasi kuwa na ubaguzi wa aina yoyote.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kisuke, Doto Misungwi, alisema ujio wa wanachama hao ndani ya chama chake ni ishara tosha kwamba Ilani ya uchaguzi inatekelezwa kwa vitendo na kuwataka wengine kujitokeza na kujiunga kwa kuwa kile walichokuwa wanakipigia kelele ndio serikali inakitekeleza sasa.