Inaripotiwa kuwa eneo la Goma, linalozungukwa na rasilimali muhimu na utajiri mkubwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ndilo kiini cha vita vinavyoendelea ndani ya taifa hilo.
Jioni ya Jumanne, Januari 28, kiongozi wa muungano wa waasi wa AFC unaojumuisha kundi la M23, Corneille Nangaa, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wameuteka uwanja wa ndege wa Goma pamoja na ndege zilizokuwamo. Taarifa hiyo imethibitishwa na vyanzo vya kidiplomasia na usalama ndani na nje ya DRC, huku ikielezwa kuwa wapiganaji wa M23 tayari wapo katika eneo hilo.
Aidha, zaidi ya askari 1,200 wa jeshi la Kongo wameripotiwa kusalimu amri kwa vikosi vya waasi wa M23. Kutokana na machafuko yanayoendelea, shughuli za kibiashara zimesimama huku hofu ikitanda miongoni mwa wakazi wa Goma.
Imeelezwa kuwa mazungumzo kuhusu ushirikiano wa maendeleo huenda yakaendelea tu baada ya Rwanda na waasi wa M23 kumaliza mzozo na kuondoka katika eneo hilo. Kundi la waasi wa M23 ni mojawapo ya zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo wenye silaha yanayoshindania ushawishi katika eneo hilo lenye utajiri wa madini.
Kwa sasa, vikosi vya usalama vya Kongo vinaendelea na juhudi za kuwadhibiti waasi hao waliotwaa udhibiti wa uwanja wa ndege wa Goma. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 2012, waasi wa M23 waliwahi kuuteka mji wa Goma kwa muda, lakini walilazimika kuondoka kufuatia shinikizo la kimataifa. Hata hivyo, walirejea mwishoni mwa mwaka 2021, wakidaiwa kupata msaada mkubwa kutoka Rwanda, kwa mujibu wa serikali ya Kongo na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED