KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amesema wanafanya kampeni nyumba kwa nyumba, shuka kwa shuka na mtaa kwa mtaa.
Makalla ambaye ni mlezi wa Mkoa wa Dar es Salaam ameyasema hayo leo ikiwa ni siku ya pili ya uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizofanyika Kigamboni, mkoani humo.
Aidha, amesema watakaoshinda kwa haki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, mwaka huu, watatangazwa.
Aidha, ameelezea umuhimu wa nafasi zinazokwenda kugombewa katika uchaguzi huo na kukuumbushia changamoto ‘panya road’ wakati wake akiwa Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam.
Amesema wakati huo waliomsaidia ni wenyeviti 564 wa mitaa yote Dar es Salaam ambao walishirikiana naye kukomesha vitendo hivyo.
“Uchaguzi huu tunakwenda kupata viongozi tunaokwenda kuishi nao kila siku. Uchaguzi huu ni muhimu ili Rais Samia Suluhu Hassan akileta fedha za zahanati viongozi hawa ndio wanaohusika.
“Lazima mwangalie ni aina gani ya wagombea ambao tukiwachagua watakuwa suluhisho la matatizo yetu na tutashirikiana nao. Tumewaletea wagombea wazuri watatuzi wa kero zetu,” amesisitiza.
Amesema wagombea hao ni muhimu kwa sababu changamoto za maendeleo viongozi watakaopatikana kupitia uchaguzi huo ndio wanaohusika katika sekta zote muhimu.
Makalla amesema wakati CCM kikiwa na ilani inayotekelezwa, wenzao wanapitia wakati mgumu katkka vyama vyao.
Amedai Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanasambaratika kwa sababu wameanza kulumbana.
“ Mwenyekiti anaongea tofauti na makamu wake tofauti, yajayo msiyashangae. Adui yako mwombee njaa. Sisi tunataka kupita kwa kishindo. Msipoteze muda wenu kuchagua wagombea ambao chama chao kina mgogoro mkubwa,” amesema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED