KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Amos Makalla, amesema matusi na kejeli havitakuwa na nafasi kwao, na kwamba watatumia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan katika kufanya kampeni za kistaarabu na kuheshimiana wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa.
Amesisitiza kuwa viongozi na wanachama wa CCM watakaopata fursa ya kuzungumza katika majukwaa ya kisiasa katika kampeni za uchaguzi huo, watajikita kueleza maendeleo yaliyofanywa na serikali ya Rais Samia katika ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa.
Makalla ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza wanachama wa CCM Wilaya ya Ilala ambako alitumia fursa hiyo kuelelezea msimamo wa chama hicho kuelekea uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
"Uchaguzi huu utaongozwa na 4R za rais ambazo ni maridhiano, ustahamilivu, mageuzi, na kujenga upya taifa. CCM inaahidi kufanya kampeni za kistaarabu, hivyo tunaviomba vyama vingine pindi ambapo kampeni zitakapoanza, twendeni na mfumo huo.
"Tujenge hoja na tutofautiane kwa itikadi kwani tuna Tanzania moja. Uchaguzi uiache Tanzania ikiwa moja yenye amani na utulivu. CCM tunavyosema ndiyo tunamaanisha," amesema Makalla.
Pia amesisitiza kuwa mambo yaliyofanywa na serikali inayoongozwa na Rais Samia, kila mwana CCM akipewa nafasi ya kuongea jukwaani ataongea mambo mengi yaliyofanywa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED