Makandarasi wameaswa kuzingatia sheria kanuni na taratibu zote zinazoongoza shughuli za ujenzi ikiwemo kusajili miradi inayotekelezwa hapa nchini.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya Mipango na Udhibiti wa Miradi ya Ujenzi (Construction Planning, Organisation and Control) yanayofanyika kwa siku tatu jijini Mwaza, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi Rhoben Nkori alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kukuza ujuzi wa makandarasi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi kuanzia mipango mizuri, mbinu za utekelezaji na mambo yote yanayowezesha mradi kutekelezwa kwa ufanisi.
"Kupitia mafunzo haya mtajifunza misingi ya kuzingatia ikiwemo umuhimu wa Makandarasi kusajili miradi yao wanayoitekeleza na si kuwasaidia Makandarasi wengine kuweka majina yao kwenye miradi ambayo hawahusiki huku wakijua ni kosa kufanya hivyo" alisema Mhandisi Nkori.
"Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa Makandarasi wote wanaoweka majina yao kwenye miradi wasiyo husika" alisema.
Mhandisi Nkori alisisitiza umuhimu wa Makandarasi hao kufanya kazi kwa weledi na kusisitiza kuwa sekta ya ujenzi si kazi rahisi bali ni sekta inayohitaji umakini mkubwa ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyostahili.
Alitumia fursa hiyo kuwaasa dhidi ya uvunjaji wa sheria za kodi akiwataka Makandarasi kuhakikisha kuwa wanatimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Alibainisha kuwa kodi inaweza kukaguliwa hadi miaka ya nyuma, na kutokuwa makini katika malipo ya kodi kunaweza kumsababishia Mkandarasi kufungiwa ama kutozwa faini kubwa baada ya kukaguliwa mahesabu yake na kufanyiwa tathimini ya kina.
“Ni lazima mkumbuke kwamba kodi inaruhusiwa kufunguliwa kwa miaka iliyopita, na mkaguzi anaweza kuangalia rekodi za nyuma. Ni muhimu tuwe na kumbukumbu sahihi ili kuepuka changamoto hizo za kodi na mahesabu”, alifafanua.
Alisisitiza pia umuhimu wa Makandarasi hao kuweka kumbukumbu sahihi za manunuzi na malipo kwa wafanyakazi, na kufafanua kuwa uandaaji wa taarifa kamili za kampuni kunasaidia kuhakikisha uwazi na kufanikisha malengo ya muda mrefu yaliyowekwa na kampuni husika ya ujenzi.
“Kuwa na biashara yenye rekodi nzuri na yenye kuendeshwa kitaalamu ndiyo njia pekee ya kukua kwa tija na kuepuka athari zisizo za lazima”, aliongeza Mhandisi Nkori.
Baadhi ya Makandarasi waliohudhuria mafunzo haya walisema imewapa fursa kubwa ya kubadilishana ujuzi na maarifa kuhusu mbinu mbalimbali katika sekta ya ujenzi ili waweze kwenda na mabadiliko ya teknolojia.
Kwa upande wake Mhandisi wa meli kutoka kampuni ya Mdau Associate Limited Abel Gwanafya alisema ameridhishwa na mafunzo hayo kwa madai kuwa yameongeza uelewa wake wa namna ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Mwenyekiti wa Chama cha Makandarasi Tanzania - Tawi la Mwanza, Mhandisi Oscar Munisi, alisema mafunzo haya yatawawezesha Makandarasi kufanya kazi zao kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko.
Mafunzo haya yamewakutanisha washiriki zaidi ya 100 kutoka mikoa mbali mbali hapa nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED