Mfanyakazi wa bomba la mafuta akutwa amefariki

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 01:11 PM Jan 24 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Janeth Magomi.
Na Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Janeth Magomi.

MFANYAKAZI wa bomba la mafuta na Mkazi wa Mtaa wa Nyasubi, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Ahmed Ally (56), amekutwa ameuawa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kisha kuacha wamemfungia kwa nje.

 

Akisimulia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyasubi, Leonard Mayala, alisema taarifa za kutokea kwa kifo hicho alizipata kwa majirani ambao Ally alikuwa amepanga nao sehemu moja baada ya kusikia harufu mbaya.

Mayala alisema alifika kwenye eneo la tukio na kukuta mlango umefungwa kwa nje na harufu ikitokea dirishani, ndipo walipotoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kahama, ambao walikwenda kuvunja mlango na kukuta mwili wa mfanyakazi huyo umeanza kuharibika.

Baadhi ya mashuhuda na majirani wa marehemu, akiwamo Dumisha Kabaula, alisema mtu huyo alitokea Dar es Salaam kuja Kahama kufanya kazi, lakini siku kadhaa bila kwenda kazini na alipomwuliza alidai anaumwa, na siku hiyo alikuwa ajiandaa kuhama lakini baada ya siku nne wakapata taarifa za kifo chake.

 Valentina Joseph alidai alikutana na Ally macho yakiwa mekundu tofauti na alivyomzoea na alipomuuliza juu ya hali hiyo alijibiwa kuwa anaumwa hivyo anataka kupumzika.

 “Tangu  siku hiyo hakuwahi kutoka ndani hadi Januari 20, mwaka huu, tulipoanza kusikia harufu kali na mlango ukiwa umefungwa kwa nje.

 Mmiliki wa nyumba aliyekuwa amepanga Ally, Michael Kamori, alisema mkataba wake ulikuwa umeshakwisha wa kuendelea kuishi kwenye nyumba hiyo na aliomba kuongezewa muda hadi Januari 20, mwaka huu, atakuwa ameshapata sehemu nyingine na kuondoka na badala yake amepata taarifa ya kifo chake.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Janeth Magomi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa mwili wake ulikuwa umeanza kuharibika akibainisha chanzo cha tukio hilo kuwa bado hakijafahamika na wanaendelea na uchunguzi.

 Alisema mwili ulichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa uchunguzi zaidi na baadaye walikabidhi kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi. 

 Aidha, Kamanda Magomi alisema mpaka sasa hakuna mtu yeyote anayeshukiwa juu ya tukio hilo na wanaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika.

 Magomi pia alisema mkazi wa Kata ya Nyihogo, Mariamu Robert (28), alikutwa amejinyonga chumbani kwake akiwa amejifungia ndani na polisi walifika na kuvunja mlango na kumtoa.  Chanzo  cha tukio hilo pia hakijafahamika na wanaendelea na uchunguzi.

 “Kujichukulia sheria mkononi ni kukinzana na sheria kwamba hakuna mtu aliyepo juu ya sheria na kila mmoja anahaki ya kuishi. Niwatake wananchi mkoani hapa hatutasita kumchukulia hatua za kisheria wale wote wanaobainika kujichukulia sheria mkononi ama kwa kuua au kumjeruhi mtu,” alisema ACP Magomi.