MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema ndani ya miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan Mkoa wa Arusha kwa ujumla hisusani jimbo lake wamekuwa wanufaika wakubwa wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Gambo ameyasema hayo leo Jumatano Februari 19, 2025 wakati akizungumza na na Wazee wa Wilaya ya Arusha huku akiwahimiza kumchagua kwa kishindo Rais Samia kwenye uchaguzi mkuu ujao, akisema mkutano mkuu wa CCM haukukosea kumpitisha kuwa mgombea pekee kwenye uchaguzi huo.
Gambo amekutana na wazee hao kama sehemu ya utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii katika kuwapatia elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ambako pia amegawa majiko ya gesi kwa wazee 182 waliohudhuria mkutano huo.
Akiitaja baadhi ya miradi hiyo, Gambo amesema kata ya Sombetini, Osunyai na Ungalimited ni miongoni mwa wanufaika wa miradi mikubwa ya barabara ikiwemo ya Mbauda Simanjiro, ambayo itajengwa kwa kiwango cha Lami kwa njia nne, suala ambalo litaondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji hasa nyakati za mvua.
Ameizungumzia pia barabara ya Kilombero mpaka uwanja wa ndege wa Arusha Kisongo ambayo ujenzi wake ulikuwa ukisuasua tangu mwaka 2020, na Rais Samia alipoingia madarakani tayari usanifu umefanyika, fidia ya Sh. Bilioni 10 imeshaanza kulipwa kwa wananchi na tayari.
"Mchakato wa ujenzi wake umeanza katika jitihada za kuondoa msongamano wa magari kwenye Jiji hilo la Arusha sambamba na kuondoa usumbufu kwa wanaofika jijini hapo kwa kutumia uwanja wa ndege wa Arusha wakiwemo watalii," amesema Gambo.
Ameongeza kuwa Rais Samia ndani ya miaka minne ya uongozi wake amefanikisha kuupeleka mradi wa TACTICS jijini humo, mradi ambao utajenga kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi Jijini Arusha.
Pia utasaidia kujengwa soko la Kilombero pamoja na soko la Morombo ambako kufikia mwezi Juni mwaka huu, mkandarasi atakuwa amepatikana na kuanza kazi mara moja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED