WAKUU wa Nchi na Serikali za Afrika wameridhia Azimio la Dar es Salaam linalolenga kuwahakikishia upatikanaji umeme watu milioni 300 barani Afrika kufikia mwaka 2030.
Viongozi hao wametaja hatua hiyo ni muhimu katika kushughulikia changamoto kubwa za nishati ambazo zinakwamisha maendeleo ya Afrika.
Yaliyomo katika azimio hilo ni pamoja kila nchi kushiriki kugharamia upatikanaji nishati ya umeme na kujenga uwezo ili kuhakikisha utekelezaji miradi ya upatikanaji umeme kwa wakati.
Azimio linasisitiza usawa wa kijinsia katika kuongeza upatikanaji nishati, hasa kwa wanawake na wafanyakazi ili kusaidia kukuza mustakabali wa nishati endelevu.
Tamko la azimio hilo linaainisha umuhimu wa kuunganisha nishati hiyo kwenye kanda za nchi hizo, kutumia vyanzo vya nishati jadidifu kama vile jua, upepo, umeme wa maji, joto la ardhi na nishati yote mchanganyiko ili kuwa na nishati imara.
Azimio hilo linatoa wito wa ushiriki mkubwa wa sekta binafsi kupitia na kuongeza ubunifu na kuweka mazingira bora ya kisheria ili kusaidia kufungua maendeleo, kuboresha miundombinu na kuleta mageuzi ya nishati kote barani Afrika.
Viongozi hao pia wamekubaliana kuundwe Tume ya Umoja wa Afrika ambayo itasaidia kuratibu na kufuatilia utekelezaji azimio hilo, shabaha ikiwa kumaliza kabisa tatizo la umeme katika nchi zao na kuimarisha uchumi wa nchi hizo.
Wamekubaliana pia kuhakikisha upatikanaji umeme na nishati safi ya kupikia, kutumia nishati mbadala na nishati mchanganyiko huku wakiongeza uhamasishaji na kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Wakuu hao wamekubaliana kuongeza ufanisi, kupanua na kuboresha miundombinu ya uzalishaji umeme, upitishaji na usambazaji nishati kwa gharama shindani na gharama nafuu katika kanda hizo.
Viongozi hao pia wamekubaliana kuweka mipango, kanuni na mifumo ya nishati inayozingatia michakato ya ununuzi shindani na wazi, kuratibu mipango ya upitishaji, viwango vya bei na kanuni za gridi pamoja na kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo.
Vilevile, wamekubaliana kuvutia mitaji kutoka sekta bianfsi na kuhakikisha fedha zinapatikana kwa ajili ya kuleta mabadiliko kwenye mifuko ya nishati, kupokeza ahadi za wadau wa maendeleo.
Azimio hilo linalenga kutekeleza mpango wa AIDA na IDF na mpango wa maendeleo wa kuwa na malengo ya muda mrefu na upatikanaji fedha kwa ajili ya miradi ya muda mrefu kuhakikisha nishati safi inapatikana.
"Wakati lengo letu likiwa ni kufikia watu milioni 300, tunapendekeza hatua madhubuti na ushirikiano wa kisiasa katika kutekeleza. Tunaomba Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuwezesha utekelezaji azimio hili kwa ajili ya kupeleka kwenye mkutano wa AU kwa ajili ya kujadili na kupitisha," inasomeka sehemu ya azimio hilo.
Mkutano wa Nishati wa Mission 300, umefanyika nchini kwa siku mbili kuanzia juzi, ukihudhuriwa na wakuu wa nchi 24 za barani Afrika pamoja na mawaziri wa nishati na fedha pamoja na viongozi wakuu wa taasisi za fedha za kimataifa. Jumla ya viongozi 2,600 wameshiriki mkutano huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED