Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha upendo wake kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha Karibu Nyumbani kilichopo Boko Temboni, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, kwa kuwapa zawadi za vyakula na vifaa mbalimbali kwa ajili ya sikukuu.
Zawadi hizo ziliwasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ambaye alizikabidhi leo kituoni hapo kwa niaba ya Rais. Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Kunenge alisema utaratibu wa Rais Samia wa kuwakumbuka watoto wanaoishi kwenye vituo mbalimbali nchini ni wa kila mwaka.
"Rais Samia ametoa zawadi hizi kwa ajili ya kuwafariji watoto wa Kituo cha Karibu Nyumbani ili nao waone furaha ya kusherehekea sikukuu," amesema Kunenge.
Zawadi zilizotolewa ni pamoja na unga kilo 100, mchele kilo 200, sukari kilo 100, mafuta ya kupikia na ya kupaka, sabuni za unga, sabuni za kuogea, sabuni za vipande, na mbuzi.
Mkurugenzi wa Kituo hicho, Ester Mwakyanjala, amemshukuru Rais kwa zawadi hizo ambazo alisema zinawapa faraja kubwa, si tu kwa watoto bali pia kwa wasimamizi wa kituo.
“Kituo chetu kilianzishwa mwaka 2013 kikiwa na watoto watatu, lakini sasa tunalea watoto 26, tukiwa na malengo ya kufikia watoto 40. Tunawafundisha watoto wetu kuishi kama familia na kuwapa elimu ya kujitegemea baadaye,” amesema Mwakyanjala.
Mmoja wa watoto wa kituo hicho, Shangwe Rogers, amemshukuru Rais Samia na Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa zawadi hizo na kuomba waendelee kuwakumbuka mara kwa mara.
Hii ni ishara ya upendo wa serikali kwa makundi maalum, ikihamasisha mshikamano na furaha miongoni mwa watoto wanaolelewa kwenye vituo vya kulelea nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED