TAMAVITA yawaomba wagombea serikali za mitaa kutowabagua wenye ulemavu

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:49 AM Nov 24 2024
Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Kelvin Nyemba.
Picha: Shaban Njia
Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Kelvin Nyemba.

Taasisi ya Maendeleo kwa Viziwi Tanzania (TAMAVITA) imewataka wagombea wanaotarajia kuongoza serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji kuhakikisha wanawajali watu wenye ulemavu kwa kuwapatia huduma bora bila ubaguzi.

 Aidha, taasisi hiyo imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha majengo ya umma yanayojengwa yanakuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Mtendaji Mkuu wa TAMAVITA, Kelvin Nyemba, alitoa wito huo wakati akizungumza na Nipashe Digital kwa njia ya simu, akifafanua namna watu wenye ulemavu wanavyoweza kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27.

Nyemba alieleza kuwa baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa waliopita walibagua watu wenye ulemavu, hasa katika kuwapatia huduma wanazostahili. Aliongeza kuwa ubaguzi huo umesababisha wengi kupoteza haki zao, ikiwa ni pamoja na umiliki wa ardhi. Aliwataka viongozi watakaochaguliwa kuhakikisha wanatoa huduma sawa kwa kila mtu bila ubaguzi.

“Katika uchaguzi huu, sisi pia tuna haki ya kuchaguliwa kama makundi mengine. Ulemavu tulionao usitumike kutunyanyapaa majukwani kwa madai kwamba hatuna uwezo wa kuongoza. Viongozi watakaopata nafasi ya kuchaguliwa wahakikishe wanatuhudumia kwa haki na heshima,” alisema Nyemba.

Nyemba aliwataka viongozi wa mitaa kuondoa vikwazo vinavyowakwamisha watu wenye ulemavu kupata mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na halmashauri. Alihimiza viongozi kusaini nyaraka zinazohitajika bila kuwatoza ada au kuwawekea masharti magumu, huku akiwashauri kushirikiana na watu wenye ulemavu katika miradi ya kiuchumi kama ujasiriamali na uchimbaji wa madini ili kuboresha kipato chao.

TAMAVITA pia iliziomba Kamati za Usalama na Tamisemi kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha usalama wa watu wenye ulemavu siku ya uchaguzi. Nyemba alisisitiza kuwa vurugu au fujo zinazoweza kutokea zina madhara makubwa kwa kundi hilo, akiwataka watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi na kuchagua viongozi bora.

James Mshima, mgombea wa CHADEMA katika mtaa wa Kagongwa, Manispaa ya Kahama, alisema kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata mikopo ya asilimia mbili ili waweze kujikimu kimaisha kupitia biashara.

Kwa upande wake, Bernardi Mapalala, mgombea wa CCM katika mtaa wa Nyahanga, aliahidi kuendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki sawa na kushirikiana nao katika kuibua miradi mipya ya kiuchumi ili kupunguza utegemezi.

TAMAVITA imesisitiza umuhimu wa wagombea kunadi sera zinazowajali watu wenye ulemavu na kuhakikisha kuwa kundi hili linapewa kipaumbele katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Viongozi wapya wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa haki na uadilifu ili kuhakikisha jamii inakuwa jumuishi kwa kila mtu.